Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imewageuzia kibao Wakala wa Serikali wa Uendeshaji wa Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka, Dar Rapid Transit Agency (DART), na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) walioishtaki kampuni ya Spark Venture (T) Limited, wakilalamikia kuvunjwa kwa mkataba wa kibiashara.
DART, msimamizi wa mfumo huo wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (Bus Rapid Transit – BRT), maarufu Mwendokasi, na AG waliishtaki kampuni ya Sparks wakiilalamikia kuwa imevunja mkataba huo wa uwekaji matangazo katika Daraja la Morocco kwa kushindwa kulipa kodi ya pango.
Katika kesi hiyo ya madai namba 9788/2024, wadai waliiomba Mahakama itamke kuwa kampuni hiyo ilivunja mkataba, iiamuru ilipe Sh89.46 milioni, ikiwa ni kodi halisi Sh84 milioni, riba Sh5.46 milioni, adhabu ya hasara, kuondoa mabango yake darajani hapo, na gharama za kesi.
Hata hivyo, kinyume na matarajio yao ya kupata hukumu yenye manufaa na nafuu hizo, Mahakama katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu, Agosti 29, 2025, imeitupilia mbali kesi hiyo, ikieleza kuwa wadai wameshindwa kuthibitisha madai yao.
Kwa kufungua kesi hiyo, wamejikuta wakijitia kitanzani, baada ya Mahakama kuitia “hatiani,” ikieleza kuwa wadai hao wenyewe ndio waliovunja mkataba huo kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi.
“Kwa kuwa wadai wameshindwa kabisa kuthibitisha madai yao kwa kiwango kinachohitajika, kesi hii inafutwa,” amesema Jaji Mkwizu, akihitimisha hukumu baada ya kujadili hoja za pande zote katika mizania ya kisheria, huku akiwaamuru wadai kumlipa mdaiwa gharama za kesi hiyo.
Juni 20, 2022, pande hizo mbili ziliingia mkataba wa upangishaji wa nafasi za matangazo katika Daraja la Waenda kwa Miguu la Kituo cha Mwendokasi cha Morocco, kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe hiyo hadi Juni 19, 2025.
Kwa mujibu wa masharti ya mkataba huo, mdaiwa, Spark, alitakiwa kulipa kodi ya upangishaji ya Sh15,000 kwa kila mita ya mraba kwa mwezi (ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani – VAT), Sh6 milioni kwa mwezi, sawa na Sh72 milioni kwa mwaka.
Agosti 24, 2023, DART ilitangaza kusitisha mkataba huo na kuitaka kampuni ya Spark kuondoa mabango yake ya matangazo iliyokuwa imeyaweka kwa madai kuwa ilipuuzia kutekeleza wajibu wake wa kulipa kodi ya pango kwa miezi 14.
Mwaka 2024, wakafungua kesi hiyo, lakini kampuni ya Spark ilipinga madai hayo, huku ikidai kuwa DART ilisitisha mkataba huo kwa sababu ilijijua yenyewe na mwombaji wa kwanza pekee.
Ilifafanua kuwa hakuna ankara sahihi za malipo zilizotolewa kama inavyotakiwa na kifungu cha 3 na 22 cha mkataba, ndiyo maana ikashindwa kufanya malipo, jambo linalofanya deni la Sh89.46 milioni lililodaiwa kutokulipwa kuwa batili.
Hivyo, iliiomba Mahakama itupilie mbali kesi hiyo, iiruhusu kuendelea na mkataba, na DART iilipe fidia ya Sh. 250 milioni kwa rasilimali na muda ilioutumia kujitetea kwenye kesi hiyo.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, wadai walimuita shahidi mmoja, Mkurugenzi wa Fedha wa DART, Deusdedit Kasmir, ambaye alisisitiza kuwa DART ilikuwa ikitoa ankara za kila mwezi.
Alidai kuwa ankara ya kwanza ilitolewa Machi 2023, ikiwa ni ya kodi ya miezi sita kuanzia Julai 2022, ankara ya pili Juni 2023 na ankara ya mwisho Agosti 30, 2023, ya miezi 14. Aliwasilisha kitabu cha kumbukumbu cha nyaraka/barua kikionyesha kuwa Oktoba 19, 2023, kampuni ya Spark ilipokea ankara na kukiri kupokea, lakini licha ya kufuatiliwa mara kadhaa kwa njia ya simu haikulipa kodi hiyo.
Spark pia ilimuita shahidi mmoja, mkurugenzi wake Joan Marydalaile, ambaye alisema Septemba 2022, miezi miwili na nusu baada ya kusaini mkataba, alipokea ankara ya Sh54 milioni, ikiwa ni kodi ya miezi tisa.
Alidai kwamba deni lake pekee lilikuwa la miezi miwili na nusu ya kodi isiyolipwa Sh15 milioni, na kwamba wadai ndio waliovunja mkataba kwa kuchelewa kutoa ankara na kuondoa mabango yake ya kibiashara, kinyume cha utaratibu na bila mashauriano.
Hivyo, aliiomba Mahakama kutupilia mbali kesi hiyo, kulipwa fidia ya miezi 33 ya usumbufu wa kesi (Sh660 milioni), fidia ya Sh250 milioni na nafuu nyinginezo.
Jaji Mkwizu alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 37(1) cha Sheria ya Mikataba, Sura ya 345 [Marejeo ya 2023], uvunjifu wa mkataba hutokea pale upande mmoja unashindwa kutimiza wajibu wake.
Amesema haipingwi kuwa mdaiwa hajalipa kodi ya pango tangu mkataba uliposainiwa Julai 19, 2022, na kwa kuwa malipo yaliyofanyika kwa miezi mitatu mfululizo, mkataba ulivunjika moja kwa moja kufikia Oktoba 22, 2022.
Jaji Mkwizu alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 23, utoaji wa ankara ulikuwa sharti la lazima kabla ya malipo kufanyika, kumwezesha mpangaji kujua akaunti rasmi ya kulipia.
Amesema ingawa mkataba ulisainiwa Juni 20, 2022, hakuna ankara iliyotolewa ndani ya muda ulioainishwa ili kuwezesha malipo ya mdaiwa.
“Ankara ya kwanza ilitolewa Machi 24, 2023, karibu miezi tisa baada ya kuanza kwa mkataba. Hii inamaanisha kwamba mdai ndiye aliyesababisha uvunjifu wa mkataba kwa kuchelewesha utoaji wa ankara,” amesema Jaji Mkwizu.