Deus Seif aibua shangwe mkutano wa hadhara akitumia Kikagulu

Kongwa. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, amelazimika kutumia lugha ya Kikagulu ili aeleweke wakati akiwaombea kura wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Seif amehutubia kwa Kikagulu jana, Septemba 7, 2025, katika mkutano wa kampeni za mgombea ubunge wa jimbo la Kongwa, Isaya Mngulumi katika Kata ya Chiwe, Wilaya ya Kongwa, eneo ambalo linatajwa kuwa lilikuwa ngome yake kabla ya kuenguliwa jina lake.

Awali, Seif alikuwa miongoni mwa wanachama 10 wa CCM walioteuliwa kugombea kwenye kura za maoni, ambapo Job Ndugai (marehemu) aliongoza kwa idadi ya kura na Seif akashika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, baada ya kifo cha Ndugai, waligombea tena na safari hii jina lake halikuteuliwa kati ya wagombea 14.

Kwenye uchaguzi wa marudio, aliongoza Mngulumi na kisha kuteuliwa. Hata hivyo, Seif amekuwa miongoni mwa waliojitoa kuhakikisha mkurugenzi huyo wa zamani wa Manispaa ya Ilala anaukwaa ubunge wa Jimbo la Kongwa.

Katika Kata ya Chiwe, ambayo inatajwa kuwa na siasa za misimamo, CCM kililazimika kumsimamisha Seif kusafisha njia na kuwashawishi watu kuunga mkono wagombea wa chama hicho na kuacha alichokiita nongwa.

“Ili uendelee lazima upate elimu na huduma za afya. Kila kitongoji na kijiji kina shule. Kata ya Chiwe kuna shule za sekondari mbili achilia mbali shule za msingi na zahanati. Na bado tunajenga kituo cha afya. Watakaotoa kura kwa CCM nyoosheni mikono, ‘akudya kunji mbona simkunyoosha, akuya hose kuya’,” amesema Seif na kushangiliwa na kundi la wananchi.

Ametolea mfano wa guta la mizigo akisema lina magurudumu matatu, lakini likikosekana moja haliwezi kufanya kazi, hivyo kwenye uchaguzi ni muhimu kupiga kura tatu kwa wakati mmoja ambazo ni Rais, mbunge na diwani.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kongwa, Mngulumi, ameomba wananchi wamwamini na kumpa kura za ndiyo ili akakamilishe miradi inayoendelea kujengwa iliyoanzishwa na Ndugai na kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara na maji.