Unguja. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk Asha-Rose Migiro, amesema chama hicho kitaendelea kuonesha mshikamano wa kisiasa na kijamii kwa wananchi katika kusimamia utekelezaji wa sera na ilani zake ili kuimarisha maendeleo ya Taifa.
Amesema hayo leo, Septemba 8, 2025 wakati akizungumza na wanachama na wapenzi wa CCM katika mapokezi ya kumkaribisha Zanzibar Ofisi Kuu za chama hicho Kisiwandui, Zanzibar, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipotangazwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni, iliyokuwa ikishikiliwa na Dk Emanuel Nchimbi, ambaye amekuwa mgombea mwenza wa chama hicho Tanzania Bara.
Migiro amesema utekelezaji wa ilani ya CCM umeendelea kuleta matokeo chanya katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo huduma za afya, elimu, miundombinu na kilimo, kwani mafanikio hayo ndiyo msingi wa chama kuelekea uchaguzi mkuu.
Dk Migiro amesema ni heshima kubwa kwa chama hicho kumpa nafasi ya uongozi wa juu, huku akisisitiza dhamira yake ya kuendeleza utekelezaji wa ilani ya CCM kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.
“Tunafahamu kuwa CCM kimeaminiwa kwa miaka mingi na wananchi. Ni wakati wa kuendelea kuinadi ilani ya CCM na kuhakikisha tunasimamia maendeleo ya Taifa letu moja lenye mshikamano, usawa na amani kwa manufaa ya wote,” amesema.
Amesema kwamba uteuzi wake ni ishara ya usawa wa kijinsia na mshikamano ndani ya CCM, akibainisha kuwa kuchaguliwa kwa mwanamke kushika wadhifa huo wa juu ni hatua kubwa ya kuendeleza sera za usawa, mashirikiano na umoja katika chama.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wanachama na wananchi kujitayarisha kwa uzinduzi wa kampeni rasmi za chama utakaofanyika Septemba 13, 2025, kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufanya uteuzi wa wagombea.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Mohamed (Dimwa), amesema wananchi wa Zanzibar hawana shaka na CCM kwa kuwa chama hicho kimeendelea kuaminika kutokana na uongozi bora wa viongozi wake, akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
“Wananchi wamemkubali Dk Mwinyi kwa uongozi wake uliotukuka. Hakuna mbadala wa ushindi wa CCM, kwani chama hiki kinakubalika kwa wananchi na kitashinda uchaguzi kwa ridhaa ya wananchi wenyewe,” amesema Dk Dimwa.
Amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ili kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana mapema kwa amani na utulivu.
Awali, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mmbeto Khamis, amesema mapokezi hayo ni heshima kubwa kwa CCM Zanzibar, hasa kuelekea uchaguzi mkuu, kwani yanaonesha mshikamano uliobebea haiba ya chama na wanachama wake.