Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika muhimili wa Mahakama, kunahitajika kuwa na taasisi imara za kusimamia changamoto za sheria zinazojitokeza katika uwekezaji.
Amesema amesema uimara wa taasisi hizo unajengwa na uwajibikaji na kuwepo kwa mazingira wezeshi ya kazi, ikiwemo ujenzi wa majengo yanayotoa nafasi ya kutenda kazi kwa ufanisi zaidi.
Dk Mwinyi amesema hayo leo, Septemba 8, 2025, wakati akifungua majengo mapya ya Mahakama za Mikoa na Wilaya, Mazizini, Mjini Unguja.
“Muhimili wa Mahakama ni moja ya taasisi zilizokuwa zinakabiliwa na changamoto mbalimbali. Hivyo, kutokana na uwekezaji unaofanywa katika muhimili huu, tunahitaji kuwa na taasisi za kusimamia changamoto za sheria, na ndio sababu ya kujenga majengo yanayotoa nafasi kwa watendaji kufanya kazi zao kwa ufanisi,” amesema Dk Mwinyi.
Ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa majengo hayo, kuna mradi mwingine wa kujenga Mahakama za Wilaya unaodhaminiwa na Benki ya Dunia (WB), ambapo utaunda muhimili wenye majengo rafiki, yenye hadhi na kuendeshwa kidijitali.
Pia, ameupongeza uongozi wa Mahakama Tanzania kwa kujenga Kituo Jumuishi cha Haki kisiwani Pemba, kitakachowasaidia wananchi kupunguza gharama za usafiri wakati wa kufuatilia mashauri katika Mahakama ya Rufaa.
Dk Mwinyi amefafanua kuwa Serikali ina mpango maalumu wa ujenzi wa ofisi za Serikali, muhimili wa Mahakama na ujenzi wa Baraza la Wawakilishi, kwa lengo la kuweka mazingira bora ya kufanyakazi.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla, amesema uwepo wa majengo hayo utarahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kwani awali vielelezo vilikuwa vikiliwa na wadudu na kukwamisha utoaji wa uamuzi katika maeneo yao.
Ameeleza kuwa kwa sasa hakuna sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao kwani tayari mazingira yao yameshaboreshwa.
Akielezea mafanikio ya Mahakama, Jaji Ramadhani ametaja kuwa ni kupungua kwa mashauri ya udhalilishaji, uwezeshaji wa wafanyakazi, matumizi ya Tehama, wananchi kujenga imani, na kuimarika kwa ushirikiano wa kitaifa na kikanda.
Akitoa maelezo ya majengo hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Kai Bashir Mbaruk, amesema wamefurahi kwa mageuzi hayo yenye lengo la kujenga mazingira wezeshi ya upatikanaji wa haki.
Amesema majengo hayo yamegharimu Sh28 bilioni, fedha ambazo zitalipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), na jengo hilo litamfanya Jaji kuwa na uwezo wa kusikiliza kesi kwa uwazi.
Pia, amesema majengo hayo hayafuti machungu na madhila waliyopitia watendaji hao, lakini yataondokana na adha za msongamano uliokuwepo awali.
Amesema amani inaendana na haki, hivyo uwepo wa mahakama hizo utaimarisha amani, umoja na mshikamano kwa wananchi wake, kwani hao ni watoto pacha wasioweza kutenganishwa.
Akizungumzia ufunguzi wa majengo hayo, Fatma Mohamed Salimu, mkazi wa Maungani, amesema hatua hiyo italeta ahueni, hasa kwa kinamama wenye watoto waliokuwa wakiwaacha kwa muda mrefu kufuatilia huduma zao.
Mohamed Omar Said amesema kuwepo kwa huduma hiyo ni faraka kwao, kwani awali walikuwa wakilazimia kufuata huduma hizo masafa marefu.
Ufunguzi wa mahakama hiyo umeenda sambamba na ufunguzi wa mahakama nyingine tatu za Mkoa wa Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, na moja ya Wilaya ya Mjini Magharibi.