FCC YAWAVUTIA WAWEKEZAJI KWENYE MAONESHO YA IATF NCHINI ALGERIA

Tanzania imejipambanua kama nchi salama na yenye ushindani katika kuvutia uwekezaji kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Barani Afrika (Intra African Trade Fair – IATF) yanayofanyika mjini Algiers, Algeria kuanzia Septemba 4 hadi 10, 2025 ambapo maonesho hayo yanawakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kujadili ushirikiano na fursa za biashara.

Katika maonesho hayo, Tume ya Ushindani (FCC) inatoa elimu kuhusu ushindani na ushajishaji wa uchumi kwenye soko nchini Tanzania.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa FCC, Bi Roberta Feruzi, alisema jukumu lao ni kuwaeleza wawekezaji kuwa Tanzania ni soko salama na lenye uwazi na ushindani wa haki.

“Tunatoa miongozo kwa wadau wanaotaka kushirikiana na kampuni za ndani katika kununua au kuungana kibiashara na tunarahisisha mchakato mzima,” alisema.

“Kupitia ushiriki wake, Tanzania inalenga kutumia IATF kama jukwaa la kutangaza fursa, kuimarisha urahisi wa uwekezaji na kufungua milango ya ushirikiano wa kibiashara barani Afrika.”

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, anaongoza ujumbe wa Tanzania. Akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Iman Njalikai, wametembelea Banda la Tanzania na kujadiliana na wawekezaji kuhusu fursa zilizopo nchini.

Taasisi nyingine zinazoshiriki ni pamoja na NEMC, TANTRADE, TMDA. TISEZA, PURA, TFS na ZIPA.