Dodoma. Mahakama Kuu Masijala Kuu Dodoma itatoa uamuzi wake Alhamisi, Septemba 11, 2025, katika kesi inayomhusu aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT–Wazalendo, Luhaga Mpina, dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kesi hiyo ipo mbele ya jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba, Evaristo Longopa, na John Kahyoza. Mpina amefungua shauri kupinga kuenguliwa na INEC katika orodha ya walioomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais wa Tanzania kwa tiketi ya ACT–Wazalendo.
Mawakili na wateja wao kwa pande zote wamekubaliana hukumu hiyo itakayosomwa saa nane mchana, huku kutakuwa na kiungo cha mtandao kwa watakaokuwa mbali.

Leo, Jumatatu, Septemba 8, 2025, kesi ilianza kusikilizwa saa 3:00 asubuhi, na kuhudhuriwa na Mpina aliyeambatana na aliyekuwa mgombea mwenza wake, Fatuma Fereji, kiongozi wa chama, Dorothy Semu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omari Shaban, na viongozi wengine kutoka mkoani Dodoma.
Wakili kiongozi wa jopo la mawakili wa ACT–Wazalendo, John Seka, ameiambia Mahakama kuwa kinacholalamikiwa sio uamuzi wa Msajili bali ni INEC kukataa kupokea fomu za mgombea. Seka amesema kulikuwa na maelekezo ya kumzuia Mpina, kitendo ambacho kimekiuka Katiba, kwa sababu chombo kilichofanya hivyo hakikuwa na mamlaka.
“Kama Msajili alikuwa na pingamizi, alipaswa kulipeleka baada ya fomu kupokelewa na INEC. Sasa tunahoji yeye mamlaka hayo aliyapata wapi?” amehoji Seka.

Amesema ibara nyingi za Katiba zilikiukwa, lakini kilichofanyika na INEC ni kupokea nakala ya barua kutoka Msajili, jambo ambalo ni kosa.
Wakili Edson Kilatu, anayemwakilisha Mpina, ameiomba Mahakama imtendee haki mteja wake huku akisisitiza kwamba hakuna mahali waliposikilizwa na INEC zaidi ya kupokea barua kutoka mamlaka nyingine kinyume na sheria.
Amesema kifungu cha 36 cha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi hakitoi nafasi ya kuzuia kupokea fomu, na alihoji tume hiyo ilitumia kifungu gani kulitekeleza hilo.
Hata hivyo, Wakili Mwanadamizi wa Serikali, Stanley Kalokola, ameiambia Mahakama kuwa haki ya kusikilizwa ni muhimu, lakini wangesikilizwa wangevunja sheria.

Kalokola amepinga kauli ya Kilatu kwamba hakukuwa na maelekezo yoyote kuhusu Mpina kuenguliwa, akibainisha kuwa kalenda ya uchaguzi imeweka muda na utaratibu wa matukio, hivyo mchakato mwingine usingezaa matunda yoyote.
Kalokola pia amesisitiza kuwa uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa haujawahi kupingwa na chombo chochote, na ACT–Wazalendo hawajasema kama mtu waliyempendekeza alikuwa na sifa za kuwa mgombea.
Shauri hilo limefunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT–Wazalendo na mgombea urais aliyeidhinishwa na chama hicho, Luhaga Mpina; dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mpina na ACT–Wazalendo wanaiomba Mahakama iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.