VIBONDE wa michuano ya Kombe la Cecafa Kagame, Garde-Cotes ya Djibout ambayo imechapwa jumla ya mabao 10-0 katika mechi mbili zilizopita, itakuwa na kibarua kizito leo, Jumatatu katika kundi A cha kukabiliana na Singida Black Stars kwenye uwanja wa KMC.
Garde-Cotes ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi msimu huu katika michuano hiyo iliyoanzishwa 1967, ilianza kwa kuchapwa mabao 4-0 na Polisi ya Kenya kabla ya kukumbana na mvua nyingine ya 6-0 kutoka kwa Coffee ya Ethiopia. Wana wastani wa kuruhusu mabao matano.
Wakati kwa Garde-Cotes, mechi hii ikiwa ni ya kukamilisha ratiba tu, Singida BS ambayo ilitoa sare dhidi ya Ethiopian Coffee na kuichapa Polisi, inahitaji ushindi ili kutinga nusu fainali ya michuano hiyo. Timu tatu zitakazoongoza makundi ya michuano hiyo na moja iyakayokuwa mshindwa bora ndio zitafuzu nusu kuwania ubingwa ambao msimu uliopita ilitwaliwa na Red Arrows ya Zambia.
Katika mechi mbili zilizopita, Singida BS imefunga mabao mawili na kuruhusu moja, hivyo licha ya udhaifu wa Garde-Cotes, Kocha Miguel Gamondi anapaswa kufanya kazi ili kupata ushindi wa pili mfululizo.
Akiongelea mechi hiyo, Gamondi alisema; “Tunaendelea kujenga kikosi, nimekuwa na uhitaji wa mechi hizi kwa ajili ya kuwafanya wachezaji wapya kuzoeana na wenzao, kumekuwa na viashiria chanya vya kuimarika kwa timu lakini bado tunakazi ya kufanya kwa pamoja.”
Gamondi amekuwa akitoa nafasi kwa kila mchezaji katika mashindano hayo hasa wapya kwa ajili ya kuzoeana na wenzao, miongoni mwao ni pamoja Clatous Chama ambaye aliicheza dhidi ya Polisi.
Wakati Garde-Cotes ikiwa na kibarua kizito mbele ya Singida BS shughuli pevu itakuwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambapo Coffee itakuwa ikikabiliana na Polisi zote zitachezwa muda mmoja.
Ikumbukwe msimamo wa kundi hilo unaongozwa Coffee yenye pointi nne sawa na Singida BS, Polisi inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu hivyo mechi baina ya miamba hiyo itakuwa ya maamuzi.
Kwa mujibu wa rekodi, hii itakuwa mara ya tatu kwa timu hizi kukutana tayari zimewahi kukutana mara mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Mara ya kwanza walitoka suluhu, Agosti 18, 2024 na waliporudiana Agosti 25, 2024 Polisi ikiwa ugenini iliibuka na ushindi wa bao 1-0.