Jesca Magufuli alivyogeuka turufu kwa CCM Kanda ya Ziwa

Dar/mikoani. Moja ya matukio yaliyoibua shangwe katika mikutano ya mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi katika Kanda ya Ziwa, ni uwepo wa Jesca Magufuli ambaye ni mgombea wa viti maalumu kupitia kundi la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Huyu ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli maarufu JPM.

Hata hivyo, Dk Nchimbi amehitisha safari ya kuzisaka kura katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Sensa za Watu na Makazi ya mwaka 2022 na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Kanda ya Ziwa inaundwa na mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu, Kagera na Mara, ina idadi kubwa ya watu.


Mikoa hiyo, huwa na nguvu za kuamua kwenye uchaguzi mkuu, hivyo Dk Nchimbi akapewa jukumu la kuanza kuzisaka kura za CCM kwenye mikoa hiyo.

Kampeni za uchaguzi mkuu zilianza Agosti 28 hadi Oktoba 28, mwaka huu na  Jumatano, Oktoba 29, 2025 itakuwa siku ya kupiga kura.

Baada ya CCM kuzindua kampeni kitaifa katika Uwanja wa Tanganyika Packers, Dar es Salaam, Dk Nchimbi na mgombea urais wake, Samia Suluhu Hassan wakagawana maeneo.

Samia akaanzia Morogoro, Dodoma, Songwe, Njombe, Mbeya na Iringa. Dk Nchimbi akasafiri hadi Mwanza kisha Mara, Simiyu, Shinyanga, Geita na kuhitimisha Kagera.

Katika mikutano hiyo, Dk Nchimbi ameeleza yaliyofanywa na Serikali ya CCM kwa miaka minne iliyopita na watakayofanya kwa mitano ijayo.

Katika mikutano hiyo, Dk Nchimbi alikuwa akitoa fursa kwa wagombea ubunge wa majimbo na wale wa viti maalumu kusalimia wananchi, mgombea wa eneo hilo alikuwa anapewa dakika chache kuzungumza.

Katika mkutano wa Isaka, mkoani Shinyanga, Dk Nchimbi alimsimamisha Jesca kuwasalimia wananchi.

Lakini kila aliposimama na kujitambulisha kuwa jina lake ni Jesca John Magufuli, shangwe iliibuka.

Huku kwa wasikilizaji unasikia walisema: “Yaani kama Magufuli kabisa,” na wengine wanasema: “Anaongea kama baba yake kabisa.”


Jesca anawaambia wananchi waendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa mgombea urais wa chama hicho, Samia anayepambana kubaki Ikulu kupitia ridhaa ya kura za Watanzania.

Jesca anasema CCM ndio chama kinachojali na kusikiliza vilio vya Watanzania, hivyo ifikapo Oktoba 29, mwaka huu, wajitokeze kwa wingi kumpigia kura mgombea wao wa urais, wabunge na madiwani wa chama hicho kwa maendeleo ya maeneo yao.

Wakati Jesca wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Isaka, walikuwa wakimshangilia huku akitoa ahadi mbalimbali.

Hali kama hiyo ilijirudia tena, katika mkutano wa Jimbo la Mbogwe alipojitambulisha: “Mimi ni Jesca John Magufuli.”

Shangwe zikaibuka, Jesca  akawaomba wananchi kuendelea kukiamini chama hicho na kukichagua kwa kura nyingi.

Baada ya kumaliza kuzungumza, Dk Nchimbi akasema Samia amemheshimisha mtangulizi wake, hayati Magufuli kwa kuendeleza miradi yote aliyoiacha katika hatua mbalimbali lakini ameisimamia na kuimaliza.

“Jesca anasimama kifua mbele kwa sababu kazi aliyoanzisha Rais Magufuli inakwenda mbele,” anasema Dk Nchimbi.

‘Ni turufu kubwa, ama kibwagizo’

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa anasema: “Watu wa Kanda ya Ziwa waliona fahari kuwa na Magufuli, utendaji kazi wake, miradi aliyoanzisha ni mambo yanayoonekana, sasa wakimwona mtoto wake anawajengea imani.”

Dk Kahangwa anasema kitendo cha Jesca kushiriki kampeni za awamu ya sita ni kwamba, familia ya awamu ya tano ya hayati Magufuli haina tatizo na awamu ya sita.

“Wale waliokuwa wanamuunga mkono Magufuli, Jesca anatumika kuwaunga mkono waliopo kwa sasa. Huwezi kuwa Mkatoliki kuliko Papa. Kama familia inamuunga mkono, wewe ni nani,” anasema.

Mhadhiri huyo anasema Jesca amekuja katika mazingira ambayo baba yake hakumjenga kuwa hivyo.

“Watu wakimwona wanadhani anaweza kuwa kama baba yake, hata baba yake hakuanza kama Rais, alianza akiwa wizarani, labda huyu binti anaweza kuwa mchapakazi.”

Anasema kujitambulisha kwa majina Jesca John Pombe Magufuli na kuibuka kwake katika mazingira ambayo baba yake hakumuandaa kuwa mwanasiasa kama viongozi wengine wanavyowaandaa watoto wao, ni turufu kwa CCM.

“Mahali popote ambako baba yake alikubalika, wakienda na huyo mtoto wanajengewa uwepo wa Magufuli na inaweza kuwa turufu kwelikweli kwa CCM, hilo limejionesha katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, kwa hiyo hata maeneo mengine inaweza kuwa hivyo,” anasema Dk Kahangwa.

“Kwa kuwa hakuandaliwa na baba yake, watu wanaona huyu haji kama tapeli, haji kama magumashi, anaweza kuwa kama Magufuli kwa sababu amekuja yeye kama yeye na kuiunga mkono Serikali ya sasa ni kuondoa maneno maneno.”

Mkazi wa Mbogwe, Frank Mashaka anasema Jesca anatoa taswira ya baba yake, ambaye walimpenda kutokana na uchapakazi wake.

“Tukimuona Jesca ni kama tumemuona baba yake, msikie anavyoongea kama baba yake kabisa, nimefurahi sana,” anasema Mashaka.

Oktoba 29, 1959, familia ya Joseph Magufuli ilibarikiwa kupata mtoto wa kiume na kumpa jina la John Magufuli.

Alizaliwa Wilaya ya Chato Mkoa wa Kagera ambayo hivi sasa ipo Mkoa wa Geita.

Harakati zake za kisiasa zilianza mwaka 1995 alipogombea kiti cha ubunge wa Chato na kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi.

 Mwaka 2000,  Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili na kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

Aidha, katika chaguzi za mwaka 2005 na 2010, aliendelea kuwania kiti cha ubunge wa Chato na kushinda uchaguzi huo na kuteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, aliyoiongoza hadi mwaka 2010.

Mwaka 2010 alipochaguliwa tena kuwa mbunge wa Chato aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, wizara aliyohudumu kwa kipindi kirefu na alisimamia ipasavyo ujenzi wa barabara nyingine nchini pamoja na madaraja.

Mwaka 2015 katika mbio za kuwania utumishi namba moja katika Ikulu, alikuwa miongoni mwa makada zaidi ya 36 wa CCM waliochukua fomu kuomba kuteuliwa.

Ndiyo mwaka ambao ulishuhudia makada wengi zaidi wakitaka kumrithi Jakaya Kikwete aliyekuwa anamaliza muda wake Ikulu.

Mwisho wa mchakato huo ulikuwa na majina makubwa ya mawaziri wakuu wastaafu, wanajeshi, wanasheria, wanadiplomasia, wanasheria na wafanyabiashara, Magufuli akaibuka mshindi ndani ya CCM na uchaguzi mkuu ulipofanyika.

Novemba 5, 2015 aliapishwa kuwa Rais wa awamu ya tano. Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akashinda tena na Novemba 5, 2020 akaapishwa.

Mwaka mmoja na ushehe akiwa madarakani kwenye kipindi cha pili na cha mwisho, akafariki dunia Machi 17, 2021 baada ya kuugua ghafla moyo.