Kachwele aanza na kishindo Marekani

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Cyprian Kachwele anayekipiga Whitecaps FC 2 amesema amekuwa na wakati mzuri tangu alipotoka kwenye kipindi cha kuuguza majeraha ya nyama za paja mwezi Juni mwaka huu.

Kinda huyo wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ aliyewahi kupita timu ya vijana ya Azam FC, huu ni msimu wake wa pili Marekani na uliopita akiwa na kikosi cha timu ya wachezaji wa akiba ya Whitecaps FC 2.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kachwele alisema amecheza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Marekani na amefunga mabao sita, jambo ambalo linamfanya aendelee kupambana zaidi kupata nafasi kwenye kikosi hicho.

Aliongeza kuwa bado anapambana kujihakikishia namba ya kudumu na hana presha ya ushindani ndani ya kikosi akiamini uwezo wake ni silaha tosha.

“Kila mshambuliaji anatakiwa kuwa na njaa ya kufunga, mimi nipo tayari kufunga kila ninapopata nafasi. Nafahamu kuwa nikifanya hivyo nitaisaidia timu na kwa upande wangu kama mchezaji itaniongezea kitu,” alisema na kuongeza:

“Naamini nipo kwenye kiwango kizuri kwa sasa, nafurahi kuona juhudi zangu zikizaa matunda. Lengo langu ni kuhakikisha kila nafasi ninayopata naitumia vizuri huo ndio msukumo wangu wa kila siku.”

Chama la Mtanzania huyo liko nafasi ya sita kwenye msimamo wa kundi B kati ya timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo maarufu MLS Next Pro, kwenye mechi 24 imeshinda 10 sare nne na kupoteza 10.