LICHA ya kuanza vizuri msimu akiwa na timu ya Aalborg BK inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Kelvin John ‘Mbappe’ amekiri ana kibarua kizito katika kikosi hicho kwa vile ushindani ni mkubwa kwenye nafasi anayocheza.
Kelvin amefunguka hayo wakati akizungumza na Mwanaspoti ambapo aliweka wazi kuwa eneo la ushambuliaji katika kikosi hicho lina washambuliaji wanne, ila anafurahia kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, licha ya kibarua kizito alichonacho.
“Ukiangalia nafasi ninayocheza tupo wanne lakini nashukuru Mungu kocha ananiamini na kila ninapopata nafasi nafanya zaidi ya anavyotaka yeye ndio maana naendelea kucheza kila mechi,” alisema Kelvin aliyezua mjadala kwa wadau wa soka kutokana na kutojumuishwa kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa mechi mbili za kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia 2026. Stars ilicheza na Congo juzi na kutoka sare ya 1-1 ugenini na kesho Jumanne itavaana na Niger katika mechi nyingine itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
“Timu yangu naiona inazidi kuwa imara japo hatukuanza vizuri kwasababu tulianza maandalizi ya msimu bila kocha mkuu mpaka mechi ya pili ya ligi ndio timu ikatangaza kocha baada ya aliyekuwa kocha wa timu kuondoka timu iliposhuka daraja,” alisisitiza Kelvin aliyeongeza kuwa kocha mpya wa timu hiyo, ametoka timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 21 ya Denmark.
Akizungumzia utofauti wa Ligi Kuu na Daraja la Kwanza alisema; “Nimecheza Ligi Kuu ya Denmark, lakini kwa maoni yangu Daraja la Kwanza ni gumu zaidi kwa sababu timu nyingi zinacheza kwa kujilinda na hawatengenezi mashambulizi kuanzia juu.
“Pia wachezaji wanacheza kwa nguvu na kazi kubwa sana tofauti na ligi kuu watu wanacheza kwa nafasi zaidi,” alisema nyota huyo aliyewahi kucheza klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ambapo kwa sasa ametupia mabao matatu kwenye mechi nane alizocheza hadi sasa.
Alisema kwa mwenendo mzuri wa timu hiyo anaiona ikipata nafasi ya kurudi ligi kuu msimu ujao.