Mirerani. Fundi ujenzi wa nyumba Mtaa wa Msikiti, Mji Mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, Salimu Kijuu (42) amefariki dunia huku kifo chake kikidaiwa kuwa na utata, baada ya mwili wake kukaa ndani kwa zaidi ya siku tatu bila kujulikana.
Mwili wa marehemu umegundulika Septemba 7, 2025 saa 7 mchana baada ya eneo alilokuwa anaishi katika Kitongoji cha Msikitini kutoa harufu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Septemba 8, 2025 amethibitisha kutokea kwa kifo hicho.
Kamanda Makarani amesema polisi wamefungua jalada la tukio hilo la kifo cha shaka na wanaendelea na uchunguzi wao ili kubaini chanzo chake.
Amesema uchunguzi wao wa awali umeonesha Kijuu hakutoka ndani kwake zaidi ya siku tatu na watu walipohisi harufu kali walitoa taarifa polisi ili kufahamu kilichotokea.
Amesema polisi kwa kushirikiana na viongozi na wataalamu wa afya walifika eneo la tukio na kukuta mwili huo.
“Nipo nje ya mkoa na hadi sasa siwezi kuzungumzia lolote zaidi ya hicho nilichokueleza, nipo nje ya ofisi sina taarifa za kutosha zaidi ya tukio hilo,” amesema Kamanda Makarani.
Hata hivyo, bado wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wamekumbwa na sintofahamu juu ya kifo hicho huku baadhi yao wakidai ameuawa kwa kipigo na wengine wanasema amekunywa sumu.
Mkazi wa eneo hilo, John James amesema watu wanapaswa kuacha vyombo vya Serikali kutoa taarifa ya ukweli kuliko kuzusha maneno yasiyokuwa na uhakika.
“Ni kweli kuna watu wawili wanashikiliwa na polisi, ila huu ni uchunguzi wa awali, hatufahamu kuwa amekunywa sumu au ameuawa ila daktari na polisi watatupa ukweli,” amesema James.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msikitini, Mweta Juma ameeleza kwamba bado hawajatambua chanzo cha kifo hicho ila wanasubiria taarifa ya polisi.
Amesema mwili wa marehemu, Kijuu umesafirishwa kwenda nyumbani kwao Kijiji cha Kinyasi wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma.