Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma leo Jumatatu, Septemba 8, 2025 inahitimisha usikilizaji shauri la kuenguliwa kwa mgombea urais aliyeteuliwa na Chama cha ACT-Wazalendo kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, utakaofanyika Oktoba 29.
Awali Mahakama hiyo ilielekeza shauri hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi na mawakili wa pande zote waliwawasilisha hoja zao kwa tarehe walizopangiwa.
Hata hivyo mahakama hiyo, inahitimisha usikilizaji wa shauri hilo leo kwa njia ya mdomo, ambapo mawakili wa pande zote watafika mahakamani kwa ajili ya ufafanuzi wa baadhi ya hoja zao za maandishi.
Shauri hilo limefunguliwa na Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa ACT-Wazalendo na mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Luhaga Mpina; dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Chama hicho kilichukua hatua hiyo kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais wa chama hicho, na wa INEC kumzuia kurejesha fomu yake ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali kuijaza.
Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura sana, chama hicho pamoja na mambo mengine kinapinga uamuzi wa INEC kumuengua mgombea wao huyo katika orodha ya wagombea wa vyama mbalimbali walioomba uteuzi wake.
Badala yake kinaiomba mahakama hiyo iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea wao huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.
Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza , lilipotajwa kwa njia ya mtandao (video conference) Septemba 3, 2025 kwa ajili ya amri muhimu, Mahakama ilielekeza lisikilizwe kwa njia ya maandishi.
Mahakama ilitoa maelekezo hayo baada ya wajibu maombi kuondoa pingamizi waliokuwa wameliibua walipowasilisha majibu yao ya maandishi na kiapo kinzani Septemba 2, 2025, wakipinga shauri hilo kusikilizwa huku wakiomba litupiliwe mbali wakidai kuwa lilikuwa na kasoro za kisheria.
Kuwepo kwa pingamizi hilo kungefanya mwenendo wa shauri la msingi kusimama kupisha usikilizwaji na uamuzi wa pingamizi hilo kwanza.
Hata hivyo kiongozi wa jopo la mawakili wa wajibu maombi hao, Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo alieleza mahakama kuwa baada ya kutafakari upya uharaka wa shauri hilo waliamua kuliondoa ili waendelee na usikilizaji wa shauri la msingi.
Hivyo mahakama ilielekeza shauri hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi, ikielekeza waombaji wawasilishe hoja zao Septemba 5 na wajibu maombi wawasilishe hoja za utetezi wao Septemba 7, 2025.
Pia Mahakama ilielekeza wadaawa wote (pande husika zote) kufika mahakamani hapo leo kwa ajili ya usikilizwaji kwa mdomo, kutoa ufafanuzi mfupi wa baadhi ya hoja walizoziwasilisha kwa maandishi.
Katika hatua hiyo Mahakama itakuwa na nafasi ya kuwauliza mawakili wa pande zote na kuwataka kutoa ufafanuzi kwa hoja ambazo itaona kuwa zinahitaji ufafanuzi zaidi, ili iweze kupata uelewa zaidi wa kilichokusudiwa.
Baada ya hatua hiyo Mahakama hiyo itapanga tarehe kwa ajili ya uamuzi wa shauri hilo ambao ndio utatoa hatima ya Mpina katika kinyang’anyiro hicho cha kugombea urais katika uchaguzi wa baadaye mwaka huu.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kuomba uteuzi wa INEC kupeperusha bendera yake katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025
Hata hivyo uteuzi wake huo ndani ya chama ulibatilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuatia pingamizi lililowasilishwa kwake na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.
Katika pingamizi hilo, Monalisa alidai kuwa uteuzi wa Mpina ni batili kwani hakuwa na sifa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Chama, Toleo la mwaka 2015, kanuni namba 16(4) (i-iv).
Pamoja na mambo mengine, alifafanua kuwa kanuni hizo zinaeleza kuwa mgombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa, anapaswa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.
Monalisa katika pingamizi lake alidai kuwa Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho, Agosti 5, 2025 na alipitishwa na mkutano mkuu kupeperusha bendera yake Agosti 6, siku moja baada ya kujiunga na chama hicho
Msajili wa Vyama vya Siasa katika katika uamuzi wake baada ya kusikiliza pande zote alikubaliana na hoja za pingamizi la Monalisa na kutengua uteuzi huo wa Mpina.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Agosti 26, 2025, Msajili alisema kuwa uteuzi ulikiuka masharti ya kifungu cha 4(5)(a) na (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258.
Alifafanua kuwa uteuzi huo uligubikwa na haukufuata misingi ya sheria, katiba na kanuni za vyama vyao kinyume na kifungu cha 6A(2) cha Sheria hiyo.
Kufuatia uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa, INEC nayo ilitangaza kumuondoa Mpina katika orodha ya walioomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi huo.
INEC, katika barua yake iliyosainiwa na Mkurugenzi wake, Ramadhan Kailima, kwenda kwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, ilieleza kuwa imeifuta barua yake ya Agosti 15, 2025 iliyohusu urejeshaji wa fomu za uteuzi iliyokuwa imempatia Mpina.
Pia INEC ilimtaka Mpina asifike katika ofisi zake siku ya uteuzi wa wagombea, Agosti 27, 2025.
Hata hivyo, siku hiyo Mpina alikwenda katika ofisi hizo kurejesha fomu yake ya kuomba uteuzi baada ya kuijaza na kutafuta wadhamini katika mikoa mbalimbali, lakini alizuiliwa na maofisa wa polisi kuingia ndani ya ofisi hizo.
Ndipo siku hiyo Agosti 27, 2025 wakafungua shauri hilo kupinga uamuzi huo wa INEC.
Shauri hilo lilipotajwa mara ya kwanza Agosti 28, 2025, waombaji waliwakilishwa na jopo la mawakili watano, John Seka, Edson Kilatu, Peter Madeleka, Mwanaisha Mdeme na Jaspar Sabuni.
Wajibu maombi wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method na mawakili wa Serikali, Stanley Kalokola na Erigh Rumisha.
Siku hiyo mahakama ilikataa maombi ya waombaji kusimamisha mchakato wa uteuzi wa wagombea wengine ikisema kuwa tayari ulikuwa umeshakamilika tangu jana yake.
Hata hivyo Jaji Kagomba alifafanua kuwa, mahakama ikijiridhisha kuwa taratibu za kisheria na kikatiba hazikufuatwa katika kuondolewa kwa mwombaji wa pili (Mpina), haki yake itarejeshwa .
Pia Mahakama kwa kuzingatia udharura wa shauri hilo iliwapa siku tano wajibu maombi kuwasilisha majibu ya madai badala ya siku 14 za kisheria walizoomba mawakili wao, ambazo pia zilipingwa na mawakili wa waombaji, waliotaka wapewe hata siku moja.