BAADA ya Simba kutangaza rasmi kuachana na aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Ally Salim inadaiwa Dodoma Jiji ilikuwa katika hatua ya mwisho ya kumbeba, japo JKT Tanzania nayo ilikuwa ikimpigia hesabu kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili usiku wa jana.
Kipa huyo aliyekuwa akisubiri mbele ya Aisha Manula, kisha Moussa Camara msimu uliopita alikuwa na mkataba mrefu na Simba, iliyotaka kumtoa kwa mkopo Namungo lakini jamaa akaweka mgomo akitaka atemwe jumla kitu kilichotekelezwa na inalezwa alikuwa Dodoma kumalizana nao.
Mwanaspoti lilipata taarifa za ndani zilizoeleza jana Jumapili jioni alikuwa mbioni kumalizana na Dodoma, japo JKT nayo ilikuwa ikitajwa ikimzivia na alikuwa akipiga hesabu kuhusu masilahi yake.
Mmoja wa viongozi kutoka JKT Tanzania alisema: “Kabla ya Simba kumalizana na Salim tuliomba tupewe kwa mkopo ila ikawa ngumu kwani mchezaji alitaka avunjiwe mkataba wake, awamu hii tunarudi kwake kwa mara ya pili hivyo lolote linaweza likatokea.
“Baada ya kumuuza Yakoub Suleiman kwenda Simba tulimsajili Ramadhani Chalamanda kutoka Kagera Sugar, lakini bado tuna uhitaji wa kipa mwingine, tukimpata Salim litakuwa jambo jema kwetu.”
Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa Dodoma Jiji ndio iliyokuwa katika nafasi nzuri ya kumnasa kipa huyo baada ya kuzungumza nao na kuelekea kukubaliana kwa ishu ya masilahi.
“Siwezi kuzungumza lolote kabla dili hilo halijakamilika, tukimsaini basi tutatangaza,” kilisema chanzo kutoka Dodoma jana mchana.
Dirisha la usajili limefungwa usiku wa kuamkia leo baada ya kuwa wazi tangu Julai Mosi mwaka huu siku chache baada ya kumalizika kwa msimu wa 2024-2025, huku Yanga ikibeba mataji yote matatu ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, huku SImba ikimaliza ya pili katika Ligi na kuishia nusu fainali ya Kombe la Shirikisho ikitolewa na Singida Black Stars.