Kocha BK Hacken amsifU Sabri

KWENYE moja ya mahojiano, kocha wa BK Hacken, Sven-Agne Larsson, amemtaja kiungo mshambuliaji wa Kitanzania, Sabri Kondo, kuwa mmoja wa wachezaji wenye njaa ya mafanikio.

Sabri, ambaye msimu uliopita alicheza Coastal Union kwa mkopo, awali alienda katika timu hiyo inayokamata nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ya Sweden, ikicheza mechi 17 na kukusanya pointi 22.

Kwenye mahojiano na kituo cha Osters IF cha Sweden, kocha huyo aliulizwa kuhusu kinda huyo na kama anaweza kumtumia kwenye kikosi chake licha ya kuwa na wachezaji wengi kwenye nafasi ya kiungo.

“Sabri ni kijana mwenye njaa ya mafanikio. Ana nidhamu kubwa. Kama kocha nafurahi kuwa na kiungo aina yake na naamini atapata jukwaa kubwa la kuonyesha kipaji chake,” alisema kocha huyo na kuongeza:

“Hadi anasajiliwa tulimuona ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, bado ni kijana mdogo. Naamini ana mengi ya kujifunza na kuhusu nafasi yake, kila aliyesajiliwa atacheza kutegemea na mpango wa mechi husika.”

Sabri anakuwa Mtanzania wa pili kucheza katika klabu hiyo baada ya awali, Aisha Masaka mwaka 2023 kukipiga akiwa na timu ya wanawake akitokea Yanga Princess.

Timu hiyo imefuzu moja kwa moja kucheza Conference League baada ya kuitandika CFR Cluj kwa jumla ya mabao 7-3 kwenye raundi ya awali ya mchujo wa kombe hilo.

Chama hilo limekuwa likishiriki michuano ya Ulaya mara kwa mara lakini halijafanya vizuri, likishia hatua za mwanzo. Kwa mara ya kwanza liliingia msimu wa 2007/2008 kwenye michuano ya UEFA Cup na likaishia raundi ya pili.

Kama timu hiyo itafanya vizuri, itakuwa sehemu ya Mtanzania huyo kuandika rekodi nyingine kwenye michuano hiyo mikubwa Ulaya, ambayo hapo awali nyota kama Novatus Miroshy na Mbwana Samatta wameweka historia.