Dar es Salaam. Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika hatua ya awali kama ilivyokuwa imepangwa.
Hali hiyo imesababishwa na mambo mapya yaliyojitokeza, ikiwamo suala la jopo la majaji na Lissu kumkataa wakili aliyeteuliwa na Mahakama kumwakilisha.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa hati ya wito kwa wadaawa, kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa leo, Jumatatu, Septemba 8, 2025, kwa ajili ya kujibu shtaka linalomkabili na usikilizwaji wa awali katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam.
Hata hivyo, kesi hiyo ilipoitwa, kuna mambo yaliyojitokeza ambayo awali hayakutarajiwa kulingana na maudhui ya hati ya wito wa wadaawa.
Mambo hayo ni pamoja na majaji wa kusikiliza kesi hiyo, mshtakiwa Lissu kumkataa wakili aliyeteuliwa na Mahakama, na Lissu kuibua pingamizi dhidi ya kesi hiyo na Mahakama yenyewe.
Awali, kwa mujibu wa hati hiyo ya wito wa kufika mahakamani, kesi ilipangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru.
Hata hivyo, leo kesi imeitwa mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde kutoka Mahakama Kuu Bukoba.
Ni takwa la kisheria, kwa mujibu wa kifungu cha 329 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023, kwa mshtakiwa anayekabiliwa na kesi yenye makosa makubwa yakiwamo ya mauaji au uhaini, kupewa na Mahakama wakili wa kumwakilisha.
Wakati kesi hiyo ilipoitwa, baada ya mawakili wa Jamhuri kujitambulisha, akasimama Wakili Neema Saruni na kujitambulisha huku akiieleza Mahakama kwamba yupo kwa ajili ya mshtakiwa.
Hata hivyo, Wakili Neema amesema baada ya kuonana na kuzungumza na mshtakiwa, amesema atajiwakilisha mwenyewe.
Baada ya maelezo hayo, Wakili Neema aliomba Mahakama impe nafasi mshtakiwa aielezee Mahakama kuhusiana na suala hilo la uwakilishi.
Lissu alipopewa nafasi, aliishukuru Mahakama kwa kumpatia wakili aliyemfuata mahabusu katika Gereza la Ukonga na kujitambulisha kwake kwamba ndiye atakuwa wakili wake katika kesi hiyo.
Hata hivyo, Lissu amesema alimweleza wakili huyo kuwa kesi inayomkabili ni kubwa, adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa, na kwa kuwa inatokana na maneno aliyoyatamka yeye mwenyewe, ameamua kujiwakilisha mwenyewe.
Amesema msaada huo wa uwakilishi huwa unatolewa kwa watu wasio na uwezo wa kupata uwakilishi au wasioweza kujitetea wenyewe, lakini yeye anaona uwezo wa kupata mawakili na pia ana uwezo wa kujitetea mwenyewe kwa kuwa yeye ni wakili wa miaka mingi.
“Hata kule Mahakama ya chini (Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu) nilikuwa nao mawakili zaidi ya 50, lakini niliwaambia wakae pembeni nikiwakilishe mwenyewe. Kwa hiyo, waheshimiwa majaji, nitajiwakilisha mwenyewe tu katika kesi hii,” amesema Lissu.
Hata hivyo, licha ya kuieleza Mahakama kwamba atajiwakilisha mwenyewe, ameieleza pia ataendelea kuwatumia mawakili wake wa awali kama wasaidizi wake kufanya utafiti wa mambo mbalimbali ya kisheria wakati akiendelea na kesi hiyo, na akaomba Mahakama iwatambue.
“Kwa kuwa Wakili Neema alishaonesha nia ya kuniwakilisha, naye akiridhia, namuomba awe kwenye timu ya mawakili wangu hawa wa kunisaidia kufanya utafiti,” amesema Lissu.
Akijibu hoja, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga amesema suala la mshtakiwa kupewa uwakilishi na Mahakama ni haki ya kisheria, lakini siyo ya lazima bali ni ya hiari.
Amesema kama hakutaka kuendelea naye, wao hawana tatizo katika hilo.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote, imekubaliana na uamuzi wa Lissu kumkataa wakili aliyepewa na Mahakama na ikaamuru aondolewe kwenye jukumu la kumwakilisha.
Kuhusu mawakili wa kumsaidia kufanya utafiti Mahakama, Jaji Ndunguru amekubaliana naye, na kuhusu Wakili Neema kuungana na mawakili wake, amesema hiyo ni ridhaa yake.
Lakini Mahakama imekataa ombi la Lissu la mawakili hao wa kumsaidia kuingizwa kwenye kumbukumbu za Mahakama ikisema hilo litaleta mkanganyiko.
Pingamizi la hati ya mashtaka
Wakili Katuga ameieleza Mahakama kuwa upande wa mashtaka walikuwa tayari kuendelea na kesi hiyo kama hati ya wito ilivyoelekeza, lakini leo asubuhi wamepokea notisi iliyowasilishwa mahakamani na mshtakiwa akipinga hati ya mashtaka na mamlaka ya Mahakama kusikiliza kesi hiyo.
Huku akirejea uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama ya Rufani, Wakili Katuga amesema linapoibuka suala la mamlaka ya Mahakama, inapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya kuendelea na mambo mengine.
Baada ya majadiliano ya muda, pande zote zimekubaliana kusikiliza kwanza pingamizi la Lissu, hususan hoja ya mamlaka ya Mahakama.
Akizungumzia hoja hiyo, pamoja na mambo mengine, Lissu amedai kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa sababu ya makosa yanayoonekana kwenye uso wa rekodi ya Mahakama ya Ukabidhi.
“Na waheshimiwa majaji, makosa haya yanaharibu utaratibu mzima wa Commital Proceedings,” amedai Lissu.
Amedai kifungu 262(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaweka masharti kuwa baada ya mtu kukamatwa na kukamilisha upelelezi, anatakiwa kusomewa shtaka lake anapopelekwa Mahakama ya chini yenye mamlaka ya eneo alilokamatiwa.
“Waheshimiwa majaji, mimi nimekamatiwa Mbinga, mkoani Ruvuma, na maelezo ya mashahidi na vielelezo yamesomwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,” amedai Lissu.
Amedai kesi hiyo imeahirishwa mara 10 katika hatua za awali kabla ya kupelekwa Mahakama Kuu, na mara zote hatua za kuahirishwa hazikuwekwa kwenye mwenendo huo.
Kabla ya kuendelea, Wakili Katuga amesema inaonekana mshtakiwa amepewa nakala pungufu kwa sababu anachokizungumza chote kipo katika nakala ya Muhtasari wa mashahidi na vielelezo.
Hata hivyo, baada ya Jaji Ndunguru kuipitia nakala aliyonayo Lissu, akabaini ni tofauti na ile iliyopo kwenye mtandao wa Mahakama na nakala hiyo haizidi kurasa 200.
Hivyo, ameelekeza itolewe nakala nyingine na apatiwe Lissu ili aipitie kabla ya kuendelea na uwasilishaji wa hoja zake, huku akimpatia saa moja ya kuipitia.
Baada ya Mahakama kurejea, Lissu aliambia jopo la majaji hao kwamba kwa muda mfupi aliosoma, amebaini kasoro nyingi kwenye mwenendo mzima. Hivyo, akaomba apewe muda zaidi wa kuipitia. Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho, Jumanne, Septemba 9, 2025.
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, maarufu kama Mahakama ya Kisutu, kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, ambayo ndio ina mamlaka ya kuisikiliza.
Anadaiwa kuwa akiwa raia wa Tanzania, tarehe hiyo, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Anadaiwa kuwa, kwa kuthibitisha nia hiyo ya uasi, alimshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kwa maneno aliyoyatamka na kuyaandika.
Hivyo, Agosti 18, 2025, Mahakama ya Kisutu, baada ya kukamilisha jukumu lake, ilihamishia Mahakama Kuu rasmi kwa ajili ya usikilizwaji kamili.