Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo anapandishwa kizimbani, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kwa ajili ya kesi ya uhaini inayomkabili, kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (preliminary hearing – PH).
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo, Jumatatu Agosti 8, 2025 katika hatua hiyo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru.
Pamoja na mambo mengine Lissu atajibu shitaka hilo kwa mara ya kwanza kabla ya kuendelea na hatua inayofuata kutegemeana na jinsi atakavyolijibu shitaka hilo,
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Anadaiwa kuwa kwa kuthibitisha nia hiyo ya uasi alimshinikiza Kiongozi Mkuu waSerikali ya Tanzania akitamka na kuandika maneno yafuatayo:
”Wakisema msimamo huu unaashiris uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutathamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shitaka hilo Aprili 10, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya uchunguzi wa awali, kukamilisha taratibu za awali ikiwemo upelelezi kabla kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya kusikiliza kesi kubwa ikiwemo hiyo ya uhaini.
Kwa kuwa mahakama hiyo ya chini (Kisutu) haina mamlaka ya kusikiliza kesi kama hiyo, siku aliposomewa shitaka hilo hakutakiwa kujibu chochote, kukana wala kukubali shitaka.
Baada ya upelelezi kukamilika na Mkurugenzi wa Mashtaka,( DPP) akaridhika na ushahidi uliopatikana, aliwasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu ambako ilisajiliwa na kuwa kesi rasmi iliyofunguliwa hapo kwa ajili ya hatua hiyo ya usikilizwaji na uamuzi.
Hivyo, Agosti 18, 2025, Mahakama ya Kisutu iliendesha mwenendo kabidhi (committal proceedings), ambapo mshtakiwa alisomewa maelezo ya mashahidi wa Jamhuri ambao inatarajiwa kuwaita kutoa ushahidi mahakamani pamoja na vielelezo vya ushahidi vitakavyotumika.
Baada ya kukamilisha hatua hizo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswaga, aliyesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya uchunguzi wa awali alitangaza rasmi kufunga jalada la kesi hiyo mahakamani hapo na kuamuru kuwa saa imeshamishiwa Mahakama Kuu.
Mshtakiwa huyo alirejeshwa mahabusu kusubiria hati ya wito wa kufika Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali kwa tarehe ambayo itapangwa.
Kwa kuwa shitaka linalomkabili halina dhamana, mshtakiwa huyo alipelekwa mahabusu ya Gereza la Ukonga anakohifadhiwa kusubiri kupangiwa tarehe ya kuitwa Mahakama Kuu kwa ajili ya hatua hiyo.
Leo Lissu atasomewa shitaka hilo kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, na kwa kuwa mahakama hiyo ndio ina mamlaka ya kusikiliza kesi yake hiyo, basi pia kwa mara ya kwanza leo atajibu shitaka hilo.
Baada ya shitaka hilo kusomwa ataulizwa na Mahakama iwapo ni kweli alitenda kosa hilo au la.
Kisha bila kujali jinsi atakavyojibu shitaka hilo, atasomewa muhtasari wa kesi, taarifa zinazojenga shitaka lake.
Kama katika kujibu kwake shitaka hilo atakiri kutenda kosa analoshtakiwa nalo, basi mahakama itamtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kosa hilo kwa mujibu wa sheria, ambapo adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Lakini kama atakana kutenda shitaka hilo, basi baada ya kusomewa muhtasari wa kesi hiyo, atatakiwa kubainisha mambo anayokubaliana nayo ( yasiyobishaniwa)na yale asiyokubaliana nayo ( yanayobishaniwa), ambayo yatasaniniwa na pande zote.
Pia Lissu atakuwa na haki ya kuwataja rasmi leo mashahidi wake anaokusudia kuwaita kumtetea, idadi na majina yao, au anaweza kuwahifadhi akawataja baadaye atakapotakiwa kujitetea.
Baada ya hatua hiyo Mahakama itapanga tarehe ya kuanza usikilizwaji rasmi wa kesi hiyo (full trial) au itaahirisha kesi hiyo kusubiri kupangiwa tarehe hiyo ya usikilizwaji.
Katika hatua hiyo ndipo Jamhuri itaanza kutoa ushahidi wake kupitia mashahidi wake itakaowaita mahakamani, hasa ikijikita katika mambo yanayobishaniwa, kuthibitisha shitaka hilo.
Wakati wa mwenendo kabidhi, kiongozi wa jopo la waendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliieleza mahakama ya chini kuwa wakati wa usikilizwaji kesi hiyo Mahakama Kuu, Jamhuri inatarajia kuwaita mashahidi 30 na kuwasilisha vielelezo tisa.
Kama kesi hiyo itaingia katika hatua ya usikilizwaji, Jamhuri baada ya kufunga ushahidi wake kwa idadi yoyote ya mashahidi itakaowaita, Mahakama itatoa uamuzi iwapo Jamhuri imejenga kesi kiasi cha kumtaka ajitetee au la.
Kama Mahakama itaona kuwa ushahidi wa Jamhuri haukuweza kujenga kesi kiasi cha mshtakiwa kulazimika kujitetea, basi itamuachilia huru na kesi itaishia hapo.
Iwapo Mahakama itaridhika kuwa kwa ushahidi huo wa Jamhuri mshtakiwa ana kesi ya kujibu basi ndipo ataanza kujitetea na kuwaita mashahidi wake kisha atasubiri hukumu ya Mahakama iwapo ana hatia au la.