Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia makada sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali na kupanga kufanya maandamano.
Maandamano hayo yalipangwa kufanyika jana, Jumapili, Septemba 7, 2025, nchini kote, ikiwa ni kuadhimisha Siku ya Mashujaa kimkoa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, ameliambia Mwananchi Digitali leo, Jumatatu, Septemba 8, 2025, kuwa wafuasi hao walikamatwa katika Kijiji cha Ndaga, Wilaya ya Rungwe, saa 6:30 mchana.
Amesema walikamatwa wakiwa wamevaa sare za Chadema pamoja na mabango, huku wakitumia mbinu ya kupita mtu mmoja mmoja kama wakiwaelekea kwenye ibada.
“Lengo lao lilikuwa ni kufanya maandamano bila kufuata taratibu za kisheria na kupelekea Jeshi la Polisi kuwatia nguvuni,” amesema.
Aidha, Kamanda Kuzaga amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa kina, na endapo utakapokamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa viongozi na wafuasi wa vyama mbalimbali vya kisiasa kuzingatia kanuni na sheria za miongozo zilizopo.
Kauli ya uongozi wa Chadema
Awali, akizungumza na Mwananchi Digitali kwa njia ya simu, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo katika vyombo vya habari.