Makamba alivyowaaga Bumbuli, amnadi Samia na mgombea ubunge

Tanga. Ni furaha na huzuni vilitawala wakati aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba aliposimama kwenye jukwaa kuwaafa wananchi hao baada ya kuwatumikia kwa miaka 15.

Huzuni na furaha hiyop ulitokana na baadhi ya wananchi kueleza jinsi wanavyokumbuka nyakati za shida na raha wakati Makamba alipokuwa akiwatumikia ndani ya miaka hiyo.

Pamoja na huzuni  hiyo, Makamba aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amewasihi wananchi wa Bumbuli kumchagua mgombea wa nafasi ya Rais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hasaan, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Radhamani Singano, diwani wa Mponde, Mbaraka Utanda.

Makamba ameliongoza jimbo la Bumbuli kuanzia 2010/2025, lakini vikao vya juu vya CCM vilimuweka kando kwenye hatua za awali mchakato wa uteuzi na kumteua Singano kupeperusha bendera.

Leo Jumatatu Septemba 8,2025 Makamba alitumia mkutano wa kumwombea kura Samia, Singano na Utanda akiwataka kuhakikisha wagombea hao wanashinda kwa kishindo.

Awali, wananchi walianza kukusanyika kwenye Kata ya Mponde eneo ambalo mkutano huo umefanyika, kuanzia saa sita ambao, ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuwaaga na kuwaombea kura wagombea wa CCM.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Makamba alitumia takriban dakika 45 akieleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongizi wake na kwamba, amefika kwa ajili ya kuwashukuru na kuwaaga rasmi.

“Nimekuja kuwashukuru kwa kunichagua kuwa mbunge wenu kwa miaka 15 na kunipa ushirikiano mkubwa ambao umetuwezesha kuwa na mafanikio kwenye jimbo letu.

“Nimekuja hapa ili tuagane rasmi, nafanya hivi kwa sababu tuliishi vizuri na kwa ushirikiano mkubwa. Upendo wenu kwangu haukuwahi kuisha, uamuzi wa vikao vya CCM, utumishi wangu kwenu kama mbunge wenu umetamatishwa,” ameeleza Makamba.

Amesema ndani ya miaka 15 kumekuwa na mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu iliyokwenda sambamba na ujenzi wa vituo vya afya.


“Wakati naanza ubunge, umeme ulikuwepo kwenye vijiji nne tu, leo vijiji vyote 84, tulikuwa na zahanati nne leo tunazo 39, tulikuwa hatuna shule za kidato cha tano na sita, leo zipo tatu.

“Kulikuwa na asilimia 22 ya wakazi wanapata maji, kwa sasa imepanda hadi asilimia 72. Tulikuwa hatuna hospitali ya wilaya, leo tunayo, hatukuwa na halmashauri, leo ipo imejengwa kwenye eneo la ekari 500 ambalo nilizitafuta, hii ni rekodi ya nzuri ya mafanikio,” amesema Makamba huku wananchi wakiwa wametulia kumsikiliza.

“Wote ni mashahidi, mmenishirikisha kwenye kila jambo na tumechangia kwa pamoja kujenga madarasa, madaraja, mifereji na rola za maji, nyumba za ibada, mitaji ya vikundi vya kina mama. Bado changamoto hazijaisha, lakini siku ya hukumu, Mungu akiniuliza kama niliitendea haki baraka ya uongozi aliyonipa, nitajibu ndio bila woga wala wasiwasi,” amesema Makamba.

Huku akishangiliwa na wananchi wa Bumbuli, Makamba alikumbushia namna ambavyo baadhi ya watu waliokuwa wakipiga picha baadhi ya maeneo jimbo hilo yenye hali duni na kueleza kuwa hakuna maendeleo yaliyofanyika.

“Mimi husema ni kweli, huo ndio uhalisia. Na hiyo ndio sababu iliyonisukuma kuomba utumishi huu ili nitoe mchango wangu kwenye kubadilisha hizo hali. Nimefanya, nimekosolewa na kusahihishwa ni ishara ya upendo, nawashukuru viongozi wote wa dini kwa ushirikiano wenu, dua na sala zenu zilinilinda.

“Ukweli sio mkamilifu na pia sikuwa mkamilifu kama mbunge wenu, hapa na pale nilifanya makosa kwa udhaifu wa kibinadamu. Kwa wale walioumizwa kwa makosa niliyoyafanya wakati nikiwa mbunge wenu, naomba leo mnisamehe, mlinipenda kwa kunikosoa na kunisahihisha.”

Amwombea kura Samia, Singano

“Mgombea wetu, mdogo wangu Singano imani yangu kuhusu uwezo wako inatokana na kwamba umeteuliwa na CCM na vikao vya juu haviwezi kufanya makosa kuhusu uwezo wa mwanachama miongoni mwetu.


 “Kwa hiyo, nimekuja hapa kuwaomba tumuunge mkono na tumpigie kura, najua mnaniamini na mnasikiliza. Najua wanadamu tunatofautiana kwa haiba na namna yetu ya kufanya mambo,” amesema Makamba na kuongeza kuwa,” Tusimtafute January Makamba ndani ya Singano. Tumpatie Singano nafasi na ushirikiano ila kutuwakilisha na kutuongoza kwa ubora zaidi kuliko nilivyojaliwa,” amesema Makamba.

Kuhusu Samia, Makamba amesema Bumbuli imepiga hatua katika safari za maendeleo chini ya uongozi wa Rais Samia kutokana na rekodi yake nzuri ya kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania.

“Mgombea wetu wa urais, Samia anaijua Bumbuli, ameshughulikia changamoto zetu ndani ya miaka minne iliyopita. Kwa rekodi ya CCM na rekodi ya Serikali, ukweli ni kuwa Samia anastahili kupata kura kwa wingi katika jimbo letu,” amesema.

Pia, ametumia jukwaa hilo kuwashukuru Marais akimtaja Samia, Jakaya Kikwete na Hayati John Magufuli kwa kumwamini na kumteua kushika nyadhifa za uwaziri kwa nyakati tofauti ndani ya miaka 12.

Amesema viongozi hao wamemjenga na kumfundisha namna ya kuwa kiongozi bora na kwamba, hatua ya kuteuliwa kwake kwenye nyadhifa hizo ni ushahidi.

Kauli za wananchi wa Bumbuli

Baadhi ya wananchi wa jimbo hilo, waliozungumza na Mwananchi wamesema watamkumbuka Makamba kwa upendo, ukarimu na maendeleo aliyoyafanya kwa miaka 15 ya utumishi wake.


“Tutakumbuka kwa mengi mambo ametufanyia, amepambana ujenzi wa vituo vya afya, hospitali na huduma za maji. Lakini, ametupambania hadi Bumbuli kuwa halmashauri sasa kwa nini tusimkumbuke,?

“Hatutamsahau ndio, ndio maana wakati anafika katika mkutano huu, baadhi ya wananchi walionekana wakitokwa na machozi na wengine kuhuzunika kwa. Huyu mgosi (Makamba) ametufanyia mengi kwenye ikiwemo afya na elimu,” amesema Paula Lubwaza.

Naye Charles Mdoe amesema: “Asiyempenda Makamba… sisi bado tunampenda na tutamuunga mkono pia Singano kwa sababu ndio ameteuliwa na chama. Amewasaidia vijana ujenzi wa vijiwe vya bodaboda ili kujinga na mvua.

 “Kikubwa Singano afuate nyayo za Makamba ambaye alikuwa karibu na watu wa jimboni hapa. Tunajua viporo haviishi kikubwa Singano ashirikiane na Makamba ikiwezekana awe naye bega kwa bega,” ameeleza.