MAKAMU WA RAIS AHUTUBIA MKUTANO WA MABADILIKO YA TABIANCHI NCHINI ETHIOPIA

………………………

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Philip Mpango amesema licha ya Afrika kuchangia chini ya asilimia nne
katika uzalishaji wa hewa chafu duniani lakini ndiyo inayoathiriwa zaidi na
mabadiliko ya Tabianchi na hivyo kuhitaji usaidizi wa haraka katika kuhimili
hali hiyo na kuhakikisha mapinduzi ya kijani.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia katika
Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Afrika kuhusu
Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia. Ametoa wito
kwa washirika wa Kimataifa kutekeleza ahadi zao za utoaji fedha katika njia
mpya na zinazotabirika kama ilivyokubaliwa chini ya Mkataba wa Paris na
kuendesha Mfuko wa Hasara na Uharibifu kwa rasilimali za kutosha.

Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuzingatia malengo ya
Kimataifa ya kuhakikisha hali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi inapewa
kipaumbele sawa na hali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema mageuzi katika
nishati ni nguzo muhimu katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi. Ameongeza kwamba, Tanzania inaendelea kuongeza uwekezaji katika
nishati jadidifu kupitia umeme wa maji, jua, jotoardhi na upepo, huku pia
ikitumia gesi asilia kama nishati safi ya mpito kusaidia ujenzi wa viwanda
pamoja na kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia, unaolenga kuhakikisha
asilimia themanini ya kaya zinatumia nishati safi kupikia ifikapo 2034.

Pia, Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea na
dhamira ya kujitolea kufanya kazi na wadau wote ili kuendeleza azma ya
kusambaza umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030 kama
ilivyodhamiriwa katika Mkutano wa Nishati wa Afrika wa Misheni 300 uliofanyika
Dar es Salaam Januari 2025.

Ameongeza kwamba Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar na
Mpango Mkakati wa Uchumi wa Buluu kwa upande wa Tanzania Bara, huimarisha
matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, pwani na nchi kavu, kusaidia ajira
na ustahimilivu katika shughuli za uvuvi, usafiri wa baharini na utalii.

Makamu wa Rais amesema Tanzania ikiwa na heshima ya
kuwa mwenyekiti wa kundi la majadiliano la Afrika kuhusu mabadiliko ya
tabianchi (AGN) kuelekea Mkutano wa COP30 nchini Brazil, itaendelea kufanya
kazi kwa bidii kuratibu msimamo wa pamoja wa Afrika na kuhakikisha vipaumbele
ya bara hilo, fedha, hasara na uharibifu pamoja na mabadiliko ya haki
yanazingatiwa katika majadiliano hayo.

Amesema Mkutano wa 30 wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko
ya Tabianchi (COP30) ili uwe na mafanikio ni lazima utoe matokeo kabambe,
jumuishi na yenye usawa. Ameongeza kwamba, Tanzania itatoa usaidizi kamili kwa nchi
ya Brazili ili kuhakikisha kuwa mkutano huo unatekelezwa kwa ajili ya Afrika na
dunia kwa ujumla.

Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendelea kukuza sauti
ya Afrika, kutafuta njia, pamoja na kufanyia kazi matokeo yenye maana ambayo
yanaakisi mahitaji ya Afrika na uwezo wake kama mshirika katika masuluhisho ya
kimataifa.

Kabla ya kuanza kwa Mkutano huo, Wakuu wa Nchi na
Serikali waliongoza zoezi la upandaji miti ikiwa ni ishara ya njia mojawapo ya
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kaulimbiu ya Mkutano huo ni Kuharakisha suluhu
za
mabadiliko ya tabianchi duniani na ufadhili kwa
maendeleo endelevu, yenye ustahimilivu na
maendeleo ya kijani barani Afrika (Accelerating Global Climate
Solutions and Financing for Africas’ Resilient and Green Development
).

Mkutano huo umetanguliwa na matukio
mbalimbali ikiwemo Wiki ya Tabianchi ya Afrika kwa mwaka 2025 iliyofanyika
kuanzia tarehe 1 hadi 6 Septemba 2025, kwa lengo la kuendeleza hatua za
kuharakisha utekelezaji wa malengo ya Mkataba wa Paris kuhusu tabianchi
.

Licha ya wawakilishi wa Serikali,
Mikutano hiyo pia imehudhuriwa na vijana, sekta binafsi, asasi za kiraia na
mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe.Hamza Hassan Juma,
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato
Chumi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi
Cyprian Luhemeja, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe. Innocent Shio pamoja
na wataalamu mbalimbali.