Mawakili waketi wakiwasubiri majaji kesi ya Mpina

Dodoma. Mawakili wa Chama cha ACT -Wazalendo na wale wa Serikali wameshaingia na kuketi kwenye viti vyao mahakamani tayari kwa ajili ya kesi ya Luhaga Mpina aliyeenguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Leo Jumatatu Septemba 8, 2025 katika Mahakama Kuu Masijala Kuu- Dodoma, majaji wanatarajiwa kutoa hukumu ya kesi hiyo ambayo imebeba hatima ya ACT -Wazalendo kama watakuwa na mgombea urais au watakosa.

Shauri hilo linalosikilizwa na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza lilipangwa leo kwa ajili ya uamuzi.

Mpina aliyepitishwa na ACT – Wazalendo kugombea urais amefungua shauri kupinga kuenguliwa na INEC katika orodha ya walioomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.

Kabla ya mawakili wa ACT – Wazalendo kuingia mahakamani hapo, walitanguliwa na mawakili wa Serikali walioingia mapema na kuanza kupekua makabrasha, dalili za kuwa wanapitia vifungu vya sheria.

‎Shauri hilo limefunguliwa na Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa na ACT-Wazalendo na mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Luhaga Mpina dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

‎Chama hicho kilichukua hatua hiyo kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wa Mpina kuomba kuteuliwa na INEC kuwa mgombea urais wa chama hicho, na wa INEC kumzuia kurejesha fomu yake ya kuomba uteuzi aliyokabidhiwa awali kuijaza.

‎Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, chama hicho kinapinga uamuzi wa INEC kumuengua mgombea wake katika orodha ya wagombea wa vyama mbalimbali walioomba uteuzi wake.

‎Badala yake kinaiomba Mahakama hiyo iielekeze INEC ipokee fomu ya mgombea wao huyo kwa ajili ya uhakiki na uteuzi.