Mechi mbili za maamuzi CECAFA

MASHINDANO ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake yanaendele leo na timu mbili zitapigania nafasi ya nusu fainali, Rayon Sports ya Rwanda itakuwa kibaruani dhidi ya Top Girls ya Burundi, huku JKU ya Zanzibar ikiumana na Yei FC ya Sudan Kusini.

Mashindano hayo yanayoendelea Nairobi Kenya, kwa siku 10, yanajumuisha timu tisa na mechi hizo mbili zitapigwa Uwanja wa Nyayo Stadium.

Kwa upande wa Rayon iliyopo kundi B, hiyo ni mechi ya maamuzi, Ushindi utaipeleka moja kwa moja nusu fainali, lakini hata sare itawapa nafasi kubwa ya kutinga hatua hiyo.

Kocha wa Rayon, Dushimimana Djamila amewataka wachezaji wake kupambania ushindi kwenye mechi hiyo na kutinga nusu fainali.

“Tunafahamu presha ya mchezo huu, lakini wachezaji wangu wako tayari, Hata kama sare inaweza kutupeleka nusu fainali, sisi tunahitaji ushindi ili tusitegemee matokeo ya timu nyingine,” alisema Djamila.

Kwa upande wa Top Girls, hii ni mechi ya kwanza kwenye kundi hilo na kocha Mpenda Mohsin alisisitiza ushindi kwenye mechi hiyo.

“Huu ni mchezo wa hadhi kubwa, tunataka kuonyesha upinzani, tunajua ugumu wa kucheza na Rayon lakini tunaamini ubora wa kikosi chetu utatupa ramani ya kwenda nusu fainali.”

Kwa jumla, mechi za leo zinatazamiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa kila upande unahitaji ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.