Mgombea  Urais CCK aahidi kukomesha njaa nchini

Arusha. Mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele, ameahidi akipewa ridhaa ya kuongoza, atahakikisha anakomesha njaa kwa Watanzania, ikiwemo kuanzisha mashamba makubwa na kusambaza chakula kwa wananchi pamoja na kutoa ajira.

Mgombea huyo ametoa ahadi hiyo leo Jumatatu, Septemba 8, 2025, akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Soko Kuu Arusha.

“Tunataka kukomesha Watanzania kushinda njaa. Watu wanakula mlo mmoja, wengine hawali kabisa. Hata ninavyosema hivi, wengine wanacheka tu kwa sababu wanapumua, lakini wana njaa kubwa na wanashida kibao.

“Kwa hiyo tumejipanga kuhakikisha jamii ya Kitanzania ina maisha bora. Raia wa Tanzania, nchi iliyobarikiwa kwanza wanakula chakula kizuri, ambacho mtu lazima ale milo mitatu, asubuhi, mchana na jioni. Hata akila mlo saa 10 akipumzika, anapoinuka kunywa uji wa ulezi na kisha ale samaki mmoja, afurahie,” ameongeza.

Amesema ili wananchi wapate chakula, wataanzisha Shirika kama lilivyokuwa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), ili kumaliza tatizo la njaa nchini, ambalo linasababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupata milo mitatu.

“Tumejipanga kuwa na shirika kubwa katika nchi hii na mikoa yote kama ilivyokuwa NMC. Walikuwa wanasaga nafaka, wanagawa na kuuza nchi nzima. CCK tutatenga mashamba makubwa ya Serikali kwa sababu tumebarikiwa na ardhi kubwa Tanzania. Tukilima mazao, tutasaga kama ni ngano, ahindi au kukoboa mpunga,” amesema.

Mgombea huyo ameahidi pia kuhakikisha sekta ya kilimo inaboresha taifa kwa kuondokana na kilimo cha analogia na kujiingiza kwenye kilimo cha kidijitali. Pia ameahidi Serikali yake kujenga nyumba na kugawa kwa wananchi kwa bei nafuu.

“Tutajenga nyumba. Najua Watanzania wengi kujenga nyumba siyo rahisi. Serikali ya CCK tutajenga nyumba na kugawa kwa wananchi kwa bei ya chini, na tutawaletea chakula kila mkoa. Hata waliopo machimbo ya Mirerani watapelekewa chini ya ardhi, wafurahie nchi yao,” amesema na kuongeza;

“Kilimo hawawezi kuwa cha mikono tu; kimepitwa na wakati. Tutalima kwa njia ya kidijitali, kilimo cha ulimwengu wa sasa. Ndiyo maana watu wanakimbia ndoa zao wakati wa kilimo, wanatorokea mjini.”

Ameahidi pia kila mwananchi, kuanzia wa vijijini hadi mijini, wapate bima za afya ili waweze kumudu gharama za matibabu, pamoja na kushusha bei ya bidhaa muhimu ikiwemo gesi, umeme na vocha, ili kila Mtanzania aweze kupata huduma hizo muhimu.

“Mikopo ya kausha damu imekausha akina mama na vijana wetu; wengine wamenyang’anywa mali zao hadi ndoa zao. Tutakomesha mikopo hiyo pamoja na kushusha bei ya pembejeo,” amesema.

Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya chama hicho, Ramadhan Bigo, ametaja changamoto zinazowakabili wananchi wa jiji hilo, ambazo akichaguliwa atazitatua, ikiwamo pembejeo, mikopo ya halmashauri kutokutolewa kwa wakati, pamoja na ujenzi wa Soko Kuu la kisasa.