Morocco yaibeba Stars, ikiifumua Zambia

LICHA ya kuwa nchi ya kwanza kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2026, Morocco jioni hii imeifumua Zambia ikiwa kwao kwa mabao 2-0 na kuilainishia Tanzania kumaliza nafasi ya pili katika Kundi E.

Mabao yaliyofungwa kila moja kipindi kimoja katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja la Levy Mwanawasa, jijini Ndola, lilififisha tumaini la wenyeji kuisogelea Tanzania itakayomalizana nao pambano la mwisho la Stars.

Youssef En Nesyri alifunga bao la kuongoza dakika ya saba, kabla ya Hamza Igamane kuongeza la pili dakika ya 47 na kuifanya Simba wa Atlas kufikisha pointi 21 kupitia mechi saba, ikiwa haijapoteza mechi yoyote kundini.

Morocco iliyoweka rekodi fainali zilizopita za Kombe la Dunia kwa kufika nusu fainali imefunga mabao 21 na yenyewe kufungwa mawili tu, ikisaliwa na mechi moja ya mwisho.

Matokeo hayo yameiacha Zambia ikibaki na pointi sita na mechi mbili mkononi. Kama Stars itapata ushindi kesho dhidi ya Niger, itaifanya ifikishe pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na Zambia kabla kumalizana.

Pointi hizo zitaifanya Stars kumaliza ya pili ya kusikilizia matokeo ya mechi ya Zambia ili kuona kama itaangukia katika timu nne za kucheza play-off kwa Ukanda wa Afrika kusaka nafasi ya kutinga fainali hizo za mwakani zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.