Lindi. Safari ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila vikwazo vya kiuchumi imeanza rasmi, baada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii 3,561, kati ya 137,294 wanaotarajiwa nchi nzima, kuanza kutoa huduma baada ya kupatiwa mafunzo na vitendea kazi.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, amesema hayo leo, Jumatatu, Septemba 8, 2025, katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa wahudumu wa afya 645 waliohitimu mafunzo hayo katika Mkoa wa Lindi.
Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku 12 tangu mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, azindue kampeni na kuahidi bima ya afya kwa wote kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake ndani ya siku 100 za kwanza iwapo atachaguliwa.
Wahudumu hao wamekabidhiwa vifaa mbalimbali, ikiwamo mizani ya kupimia uzito, mabuti, mwamvuli, begi, vipimo vya presha, sukari na joto, vifaa vya kupima damu, kifaa cha kupima hali ya lishe kwa watoto, pamoja na kishikwambi.
Dk Magembe amesema vifaa hivyo vitatumika kutoa huduma za awali, kinga, na uchunguzi wa magonjwa katika hatua za mwanzo, huku taarifa zikiwa zinaingizwa kwenye mfumo maalumu kupitia vishikwambi.
“Serikali imeingia kwenye mpango wa bima ya afya kwa wote kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bila kikwazo cha gharama. Huduma zitazingatia ubora, upatikanaji na kupunguza gharama, na wahudumu hawa wa ngazi ya jamii ndiyo watakaokuwa kiungo cha kwanza cha utekelezaji,” amesema.
Amesema wahudumu hao wamepatiwa mafunzo ya kwenda nyumba kwa nyumba kutoa elimu kuhusu bima ya afya, huduma za awali na ushauri wa matibabu, hatua ambazo ni maandalizi ya utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Aidha, amewataka wahudumu hao kuzingatia maadili ya kazi, kutumia lugha na kauli nzuri kwa wananchi, pamoja na kutoa huduma bila upendeleo.
Kwa mujibu wa Dk Magembe, pamoja na kutoa tiba na kinga, ustawi wa jamii na huduma za lishe, kila mhudumu atarekodi huduma alizotoa katika kaya husika, idadi ya watu waliopatiwa huduma, na aina ya huduma husika, ili Serikali ipate takwimu sahihi kwa urahisi.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo umeanza katika mikoa 12 na halmashauri 25, ikiwamo Lindi Mjini, Mtama, na Ruangwa.
“Hadi sasa tuna jumla ya wahudumu 3,561 waliokamilisha mafunzo ya miezi sita kwa awamu ya kwanza katika mikoa 12. Mkoa wa Lindi pekee una wahudumu 645 waliomaliza mafunzo hayo. Lengo la Serikali ni kufikia wahudumu 137,294 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ndani ya miaka mitano, kwa wastani wa wahudumu 27,324 kila mwaka,” amesema.
Amesema ukamilishwaji wa mpango huo utasaidia kugundua wagonjwa katika hatua za awali, kupunguza udumavu, utapiamlo na vifo vya mama na mtoto.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Zuwena Jiri, amewataka maofisa maendeleo na ustawi wa jamii kushirikiana na wahudumu hao kwa kuwa wamekuja kuongeza nguvu ya utoaji huduma.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakutana na mhudumu wa afya hata kabla ya kufika kituo cha kutolea huduma. Huu mpango si mpya, ulianza tangu miaka ya 1970, ila wakati huo changamoto ilikuwa uratibu na usimamizi. Sasa mfumo umeimarishwa ili ifikapo mwaka 2030 dhana ya afya kwa wote iwe imefikiwa,” amesema Jiri.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Heri Kaja, amesema katika halmashauri tatu za mkoa huo, kila kitongoji kimepewa wahudumu wawili wa kiume na wa kike, na hivyo kufikia jumla ya wahudumu 2,368.
Kati yao, 645 wamehitimu awamu ya kwanza, huku 591 wakiendelea na mafunzo ya awamu ya pili. Aidha, waliomaliza awali walikabidhiwa baiskeli za kisasa 643 kwa ajili ya kurahisisha huduma.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkapa Foundation, Zawadi Dakika, amesema taasisi hiyo imetoa vishikwambi ili kusaidia ukusanyaji wa takwimu muhimu za afya.
Akisoma risala kwa niaba ya wenzake, mhudumu wa afya ngazi ya jamii, Dickson Mahuchila, amesema vifaa vya kielektroniki walivyokabidhiwa vitawasaidia kuhudumia jamii kwa ufanisi zaidi kupitia maarifa waliyopata kwenye mafunzo.
“Tunaahidi kufanya kazi kwa moyo, weledi na maarifa ili kufanikisha matokeo chanya yaliyokusudiwa, hususan katika lishe, huduma za mama na mtoto, vijana na makundi maalumu, sambamba na kutoa elimu ya kinga na usafi wa mazingira,” amesema.