Mbeya. Mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Mapambano wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya, Athuman Mwasomora (11), amefariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kamba ya begi kwenye fremu ya mlango ndani ya chumba alichokuwa akilala.
Kufuatia tukio hilo mama mlezi wa mtoto huyo Mariam Mwakasusa (38) anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amebainisha hayo Septemba 7, 2025 na kuongeza kuwa, tukio hilo lilitokea Septemba 2, 2025 saa 4.30 asubuhi katika Kijiji cha Lulasi, Kata ya Mpombo Halmashauri ya Busokelo Wilaya ya Rungwe.
Kuzaga ametoa taarifa hiyo kufuatia kuonekana picha mjongeo ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha Ester Pangapanga (28), ambaye mama mzazi wa marehemu akidai mtoto ameuawa.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, lilianza uchunguzi wa kisayansi kwa kushirikiana na daktari wa Kituo cha Afya Ruangwa Halmashauri ya Busokelo Wilaya ya Rungwe.
“Uchunguzi ulifanyika eneo la tukio na kubaini marehemu alijinyonga ndani ya chumba alichokuwa akilala kwa kutumia kamba ya begi aliyofunga kwenye fremu ya mlango,” amesema .
Kamanda Kuzaga amesema polisi wanaendelea na uchunguzi na kumshikilia mama mlezi wa marehemu kwa mahojiano zaidi.
Baadhi ya wakazi mkoani hapa, wameiomba Serikali kupitia wizara husika kuja na mkakati wa kuwachukulia hatua wazazi wanaokimbia kutunza watoto na kuwatelekezea wazee vijijini.
“Matukio ya watoto kujikatisha uhai hayatakoma endapo sheria ya kudhibiti wazazi wanaotelekeza watoto kwa sababu zisizo za msingi na kusababisha kuishi mazingira magumu kwa kukosa matunzo na malezi bora,” amesema Sikujua Aloyce.
Amesema Serikali ikija na mkakati itakuwa suruhisho la wazazi kujua majukumu yao ya kutunza familia zinazo wategemea na sio kutelekeza kwa vikongwe vijijini na kuwa mzigo kutokana na hali duni ya maisha.