Namna ya kumsaidia mtoto anayemaliza darasa la saba

Dar es Salaam. Wakati wanafunzi wa darasa la saba wakitarajia kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi Septemba 10 na 11 mwaka huu, wadau wameainisha njia nzuri ya kuishi nao kwa miezi mitatu ijayo.

Kipindi hiki cha likizo kinatajwa kuwa fursa nzuri kwa wazazi na walezi kusaidia kukuza vipaji vya watoto wao, hivyo kupata nafasi ya kugundua na kuviendeleza, kama vile uchoraji, uimbaji, michezo, uandishi au teknolojia.

Hilo litawezekana si kwa kupeleka watoto katika masomo ya kuandaa kuingia kidato cha kwanza pekee (pre-form one), bali kuwatafutia namna wanayoweza kujifunza zaidi katika yale wanayoyapenda ili yawasaidie baadaye.

Ili kufanikisha hili, wazazi wameshauriwa kuwasikiliza watoto ili kujua wanachopenda na kuwaongoza bila kuwabana. Vipaji vikiendelezwa mapema huweza kuwa msingi wa mafanikio ya baadaye.

Wanafunzi wanaomaliza darasa la saba mwaka huu walianza safari yao ya masomo mwaka 2019, na safari yao ya elimu ya msingi inafikia tamati siku tatu zijazo.

Akizungumza na Mwananchi, mdau wa elimu, Nicodemus Shauri, amesema kwa watoto wa vijijini wengi wamekuwa wakiingia katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo ufugaji na kilimo, lakini wale wa mjini ndiyo sana wanahitaji shughuli mbalimbali, ikiwemo masomo ya kujiandaa kwenda kidato cha kwanza.

Kwa upande wake, ameshauri kuwa muda huu ni mzuri kwa watoto kupelekwa wakasome kozi fupi za vitu wanavyopenda, kama muziki (wajifunze kupiga vyombo au kupamba), kupika keki, kitu ambacho kitamsaidia baadaye.

“Wale ambao hawajui nini wanakipenda wanaweza kupelekwa katika masomo ya ziada, lakini kwa sasa dunia inavyokwenda ni vyema kuwaanzishia watoto elimu ya amali, kwani kuna watoto wengine hawana uwezo wa kwenda taaluma, na wanapenda michezo, wapelekwe huko,” amesema Shauri.

Amesema kipindi hiki pia ndiyo ambacho mzazi anaweza kubaini kipaji kingine cha mtoto wake na kumsaidia vyema ili afikie malengo yake siku za usoni.

“Kwa sababu kama ni pre-form one si mbaya, lakini watajifunza masomo hayo watakapoanza shule Januari, hivyo bora ajifunze kitu mbadala,” amesema.

Mhadhiri msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Valerius Haule, amesema wakati huu ni vyema kuwaacha watoto wapumzike baada ya mtihani, kwani shule nyingi nchini wanafunzi husoma mfululizo, hata wakati wa likizo, hawapumziki.

Hiyo hufanya mtoto kwenda shuleni mwaka mzima, hali inayofanya muda mwingi kutumia katika masomo badala ya stadi za maisha, jambo linalofanya washindwe kufanya baadhi ya majukumu ya kijamii.

“Kipindi hiki ni vyema kumuacha mtoto atilize akili. Hata akifaulu awe na ari mpya ya kwenda shule. Hiki ni kipindi ambacho mzazi anaweza kumfundisha mtoto stadi za maisha anazoweza kuzitumia wakati mwingine akiwa peke yake,” amesema.

Amesema watoto wengi wa mjini wamekuwa hawamudu baadhi ya majukumu na kushindwa kufua hata nguo zao, hawawezi kupika bila kujali jinsia, hivyo kipindi hiki ndiyo mzazi anaweza kumfundisha mtoto maadili na maisha ya ujana anayoyaelekea, ili ajue hatima yake.

“Sikubaliani sana na kumpeleka mtoto pre-form one,” amesema Haule.

Mdau wa elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema baada ya mtihani mtoto huanza kujiandaa kwenda kidato cha kwanza, lakini ni vyema watoto wapelekwe kujifunza maarifa tofauti na yale aliyopata shule ya msingi au atakayopata kidato cha sekondari.

“Kuna baadhi ya wazazi huwa wanawapeleka watoto wao kuanza pre-form one, lakini inaweza isimsaidie mtoto, kwa sababu masomo atakayosoma huko atakwenda kufundishwa kidato cha kwanza.

“Japokuwa itamsaidia kuelewa kwa upana, lakini huko kwenye vituo kumekuwa na mitaala ambayo haiendani na kile kitakachofundishwa shuleni,” amesema.

Amesema hali hiyo itamfanya mzazi kupoteza hela zake kwa kulipia masomo hayo ambayo hayawezi kumsaidia mtoto katika masomo yake ya baadaye.

“Ndiyo maana naona ni vyema kumpa mtoto kujifunza vitu vingine, kama mapishi, kutunza bustani, badala ya kupelekwa kukalilishwa nini maana ya baiolojia au kemia, kitu ambacho atakacho jifunza atakapojiunga kidato cha kwanza,” amesema.