Nangu afichua ishu yote Simba

BEKI mpya wa kati wa Simba, Wilson Nangu bado hajaungana na timu hiyo tangu alipotangazwa kutua hapo, lakini anajua kesho Jumatano katika tamasha la Simba Day itakuwa ni fursa yake kuungana na wenzake na kutambulishwa mbele ya mashabiki na anajua shoo ya tamasha hili ilivyo.

Simba inafanya tamasha hilo kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikitumika kama sehemu ya kutambulisha jezi na kikosi kipya cha msimu na Nangu alisema anamini itakuwa mwanzo wa kuongeza thamani katika maisha ya soka na anafurahia kuanzia tamashani.

Nangu ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao mawili, asisti mbili akiwa JKT Tanzania, alisema alikuwa analitazama tamasha la Simba Day na sasa anakwenda kuwa sehemu ya kikosi hicho, jambo ambalo linampa hamasa ya kujituma zaidi na furaha ya kukutana na mashabiki laivu.

“Tamasha la Simba Day linawakusanya pamoja mashabiki wa timu hiyo, kama mchezaji nategemea wanisapoti kazi zangu, hivyo naamini nitapata wakati mzuri wa kufurahia pamoja nao nikiwa sehemu ya timu,” alisema Nangu na kuongeza;

“Ni ndoto ya kila mchezaji kusapotiwa, kwanza vaibu la mashabiki linaongeza morali ya kujituma kuhakikisha hatuwaangushi uwanjani, hivyo kwangu itakuwa siku ya tofauti sana.”

Alisema ni raha mchezaji kutambulishwa mbele ya umati ambao unashabikia timu hiyo.

 “Nina maana kwamba klabu kama Simba unapojiunga nayo ukipambana thamani inakuwa juu zaidi.”

Mbali na hilo alizungumzia kujumuishwa katika kikosi cha Stars tangu kilipokuwa kinacheza michuano ya CHAN 2024 na sasa kufuzu Afcon kunavyomsaidia kumjenga na kupambana zaidi.

“Wachezaji Tanzania wapo wengi unapopata nafasi ya kulitumikia taifa lako ni heshima kubwa pia tunakutana wachezaji kutoka timu tofauti na kila mmoja ana uwezo na ubora wake,” alisema Nangu aliyesaini miaka mitatu kuitumikia Simba. Kabla ya kutua JKT Tanzania, Nangu alikuwa akiitumikia TMA Stars iliyopo Ligi ya Championship.