Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akitarajia kupandishwa kizimbani leo katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja au maelezo ya awali ya kesi ya uhaini inayomkabili, ulinzi umeimarishwa kuanzia nje, getini hadi ndani ya Mahakama.
Ulinzi huo umeimarishwa na askari wa Jeshi la Polisi waliovaa sare, na askari kanzu wakiwa wanazunguka katika eneo hilo.
Mwananchi imeshuhudia magari zaidi ya saba, yakiwemo magari mawili ya kubeba wagonjwa na gari moja la maji ya kuwasha, yakiwa wameegeshwa nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, huku yakiwa na askari waliovalia sare za jeshi hilo.
Kati ya magari hayo, mawili ni ya kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Toyota HardTop rangi nyeupe, ubavuni wakiwa na ufito wa rangi nyekundu na maandishi makubwa ya Polisi, yameegeshwa nje ya mahakama huku askari wawili waliovalia sare za jeshi wakiwa nje ya magari yao, wamevalia makoti ambayo hutumiwa na madaktari na manesi wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa hospitalini.
Hii ni mara ya kwanza kwa magari hayo ya kubeba wagonjwa ya Jeshi la Polisi kuegeshwa nje ya viunga vya Mahakama hiyo. Pia kuna gari moja la maji ya kuwasha limeegeshwa umbali wa mita 100 kutoka lango la Mahakama Kuu.
Mbali na ulinzi kuimarishwa, mtu anayeingia ndani ya Mahakama anatakiwa ajitambulishe, kuwaeleze askari juu ya kesi anayohudhuria, kisha kuguliwe na askari waliopo langoni kuu la kuingia Mahakama na kujiandikisha kwenye kitabu cha mahudhurio kilichopo getini hapo.
Vile vile, ulinzi umeimarishwa katika barabara inayolekea Kivukoni kutoka Posta ya Zamani, ambapo magari mawili ya jeshi yameegeshwa mkabala na Kituo cha Mwendokasi cha Posta ya Zamani, huku kukiwa na askari kadhaa eneo hilo.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa leo, Jumatatu, Septemba 8, 2025, katika hatua ya maelezo ya awali, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Iringa, Dunstan Ndunguru.
Pamoja na mambo mengine, Lissu atajibu shtaka hilo kwa mara ya kwanza kabla ya kuendelea na hatua inayofuata, kutegemeana na jinsi atakavyolikibu shtaka hilo.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025
Anadaiwa kuwa, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Anadaiwa kuwa kwa kuthibitisha nia hiyo ya uasi, alimshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali akitamka na kuandika maneno yafuatayo: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tuthamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025, katika Mahakama ya Kisutu.
Mpaka saa 6:13 mchana, kesi hiyo ilikuwa bado haijaanza kusikilizwa, licha ya wafuasi na wanachama wa chama hicho kujaa katika ukumbi namba moja uliopo Mahakama hiyo, pamoja na ukumbi uliopo juu, ambao hutumika kama eneo la chini, kuwa limejaa.
Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi…