DIRISHA la usajili lilifungwa usiku wa jana, huku kukiwa na sapraizi kubwa kwa klabu ya Simba baada kuwatema mastraika wawili walioibeba timu hiyo msimu uliopita, huku winga aliyekuwa akitajwa huenda angefyekwa, akisalimika kama utani.
Simba iliyotangaza sura za kazi kwa kuwarejesha vigogo wa maana katika safu ya uongozi ya Bodi ya Wakurugenzi akiwamo Barbara Gonzalez, Crescentius Magori, Azim Dewji na Swedy Nkwabi imesajili wachezaji 12, huku ikiwatoa wachezaji kadhaa kwa mikopo katika timu mbalimbali.
Ipo hivi. Msimu uliopita, Simba iliongozwa eneo la mbele la ushambuliaji na Steven Mukwala na Leonel Ateba kila mmoja akifunga mabao 13 sawa na aliyomaliza nayo Jonathas Sowah aliyekuwa Singida Black Stars kabla ya kutua Msimbazi kwa ajili ya kikosi cha msimu ujao. Nyota hao wawili kila mmoja pia aliasisti mara nne, lakini timu ikiwa kambini Misri, Ateba aliaga baada ya kupigwa bei Al Shorta ya Iraq kisha akashushwa Seleman Mwalimu ‘Gomes’ kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco.
Hivi unavyosema taarifa hii ni kwamba mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakimalizia dili la kumuuza Mukwala kwa klabu ya Al Ittahad ya Libya kabla ya dirisha hilo kufungwa usiku wa jana, lakini winga aliyekuwa akielezwa atatolewa Joshua Mutale amesalimika kufyekwa.
Simba iliamua kumuuza straika huyo wa kimataifa wa Uganda, ikiwa tayari ina Sowah na Gomes kikosini ambao pia wanachezaji nafasi hiyo ya ushambiliaji wa kati.
Mwanaspoti ilizinasa mapema jana kabla ya dirisha la usajili kufungwa usiku wa jana kwamba Mukwala amepigwa bei Al Ittihad ya Libya na ilikuwa inasubiriwa tu kutangazwa rasmi.
Mukwala msimu uliopita licha ya kutumika kwa dakika chache, taarifa zilidokeza kuwa hatakuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu ujao 2025/26.
Inaelezwa Simba ilipokea ofa ndefu kutoka Al Ittihad ya Libya ya kutaka kumnasa mshambuliaji huyo ili aitumikie timu hiyo kwa msimu huu na mabosi wa Msimbazi hawakuona hiyana kumuachia.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti, Al Ittihad, ilifika dau la kumnunua mshambuliaji huyo na dili hilo linatajwa kukamilika jana na kilichokuwa kinasubiriwa ni uthibitisho kutolewa na kuifanya timu kuwaondoa mastraika wake wote kwani Mashaka Valentino amepekwa kwa mkopo JKT Tanzania kama ilivyo kwa Saleh Karabaka, David Kameta ‘Duchu’ na Awesu Awesu.
“Ni kweli tumefikia makubaliano ya kumuuza Mukwala kwenda Al Ittihad na kuna uwezekano akasajiliwa mchezaji mmoja ambaye atapishana na Mukwala kama kocha alivyosisitiza kuongezwa mchezaji mmoja,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Tumemuuza Mukwala kwa dau nono sana siwezi kuweka wazi ni kiasi gani lakini pesa hiyo itatusaidia kunasa saini ya mchezaji mwingine yeyote bora kama ambavyo kocha Fadlu amesisitiza kusajiliwa mchezaji mwenye ubora mkubwa.”
Mukwala ambaye wakati anatua Simba iliripotiwa amesaini mkataba wa miaka mitatu, tayari ametumikia mwaka mmoja na kuisaidia timu hiyo kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco.
“Makubaliano ya pande zote mbili kati yetu sisi Simba na Al Ittihad yanakwenda vizuri nafikiri taarifa ya usahihi zaidi kama dili limekwenda kama lilivyopangwa kesho (leo) itatolewa na kila mwanasimba ataupongeza uongozi kwa biashara nzuri tuliyoifanya.”
Hivi karibuni kocha, Fadlu alisema bado wanahitaji angalau mchezaji mmoja mwenye kitu cha ziada. (X-Factor) atakayewaongezea kitu hasa kwenye michuano ya kimataifa pamoja na mbio za ubingwa wa ligi.
Kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili jana usiku, Simba ilikuwa imesajili wachezaji 12 wakiwamo sita wa kigeni, Rushine de Reuck, Neo Maema, Mohammed Bajaber, Naby Camara, Jonathan Sowah na Alassane Kante.
Wachezaji wengine sita ni wazawa ambao ni; Gomes, Morice Abraham, Wilson Nangu, Yakoub Suleiman, Charles Semfuko na Anthony Mligo.