Kyiv, Ukraine. Watu wanne, akiwemo mama na mtoto mchanga, wamefariki dunia huku wengine 18 wakijeruhiwa kufuatia shambulio la anga lililofanywa na vikosi vya Urusi nchini Ukraine.
Kwa mujibu wa Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, mashambulizi hayo yamefanyika usiku wa kuamkia leo, yakihusisha ndege zisizo na rubani na kufuatiwa na makombora yaliyolenga maeneo ya makazi
Klitschko amesema idadi kubwa ya vifo na majeruhi imesababishwa na kuta za majengo kuanguka baada ya kushambuliwa.
“Urusi ilikuwa ikilenga raia kwa makusudi bila kuzingatia utu wa kibinadamu wala huruma kwa wakazi wa maeneo hayo,” amesema.
Amefafanua kuwa mabaki ya ndege zisizo na rubani yaliyodondoka kwenye majengo ya makazi yalisababisha moto kuwaka katika jengo la ghorofa 16 pamoja na majengo mawili ya ghorofa tisa na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Moto huo pia umeathiri shughuli za uokoaji kutokana na moshi mzito uliotanda na kusababisha sakafu za majengo kadhaa kuharibika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala wa Jiji la Kyiv, Tymur Tkachenko, amesema mashambulizi hayo pia yameharibu miundombinu ya usafiri katika mji wa Oleksandr Vilkul kutokana na mtetemo wa makombora.
Hata hivyo, Jeshi la Urusi halijatoa taarifa ya moja kwa moja ya kuhusika na mashambulizi hayo, ingawa Serikali ya Ukraine imeripoti kuwa ni vikosi vya Urusi vilivyohusika.
Tukio hilo pia limezifanya nchi jirani za Ukraine, ikiwemo Poland, kuongeza ulinzi wa anga zikihofia kuathiriwa na mapigano yanayoendelea baina ya Urusi na Ukraine.
(Imeandikwa na Elidaima Mangela, kwa msaada wa mashirika ya habari)