Karatu. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimesema kikipata ridhaa ya kuunda Serikali baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 , 2025 kitaweka mfumo wa haki wa usimamizi wa bei ya mbaazi ili kuwainua wakulima mkoani Manyara na maeneo mengine nchini.
Akizungumza katika mkutano kampeni na wananchi wa Kijiji cha Chemchem, leo Jumatatu Septembva 8, 2025 mgombea urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amesema mfumo huo utawawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika kupanga bei ya mazao bila kuingiliwa na madalali au maofisa wa Serikali wasiowajali wakulima.
“Serikali yangu haitakubali udalali wa kuuza mazao, si mbaazi tu bali mazao yote. Madalali wanawanufaisha wao binafsi na kuwaacha wakulima katika umaskini. Serikali inayojali haiwezi kukaa kimya huku wananchi wake wanauza kilo ya mbaazi kwa Sh400,” amesema Mwalimu.
Kwa sasa, wakulima wa mbaazi mkoani Manyara wanauza kilo moja ya zao hilo kati ya Sh400 hadi Sh500, ikilinganishwa na Sh1,600 hadi Sh1,800kwa msimu kama huu mwaka jana.
Hali hiyo imewakatisha tamaa wengi, wakiwamo wakulima kama Martin Kaisei ambaye amesema ugumu wa soko na kushuka kwa bei, kumeathiri ustawi wa kilimo hicho.
“Bei hii ni ya aibu, haiwezi hata kurudisha gharama ya kuandaa shamba. Tunalima kwa nidhamu na juhudi, lakini hatuoni matunda yake,” amesema Kaisei.
Ameongeza kuwa, licha ya matumaini waliyoyapata kupitia sera za mgombea wa Chaumma, bado wana wasiwasi kuhusu utekelezaji wake kutokana na ahadi nyingi walizowahi kupewa na viongozi waliopita.
Mwalimu amesema mbaazi ya Tanzania inauzwa katika masoko ya kimataifa kama India, China na Uingereza, hivyo haiingii akilini kuona wakulima wakipata bei ya chini ilhali mahitaji ya kimataifa ni makubwa.
“Haiwezekani mbaazi inayotoka Tanzania inauzwa nje ya nchi kwa bei nzuri lakini hapa nyumbani mkulima analipwa Sh400 kwa kilo. Hii ni sawa na kutaka kuwaangamiza wananchi wako kwa makusudi,” amesema.
Chaumma imeahidi kuweka mazingira ya kisheria na kisera yatakayompa mkulima nafasi ya kuamua bei ya mazao yake, ikiwa ni pamoja na kupambana na urasimu na udalali kwenye minyororo ya masoko ya kilimo.