ULEGA AOMBA KURA KWA AJILI YA DKT. SAMIA, UBUNGE NA MADIWANI MKURANGA

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga, Mkoa wa Pwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Alhaj Abdallah Ulega, leo Jumatatu Septemba 8, 2025 ameendelea na mikutano yake ya kampeni kwa kuwahutubia wananchi wa Kijiji cha Bupu katika mkutano wa hadhara.

Katika hotuba yake,Ulega alianza kwa kuwaomba wananchi waendelee kumuamini na kumpa kura za kishindo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Aidha, aliomba kura kwa ajili ya wagombea ubunge na udiwani wa CCM wilayani humo, akisisitiza mshikamano wa chama hicho ni nguzo muhimu ya kuleta maendeleo ya wananchi.

Katika mkutano huo, Ulega pia aliwanadi wagombea udiwani wa kata mbalimbali za Wilaya ya Mkuranga, akiwataka wananchi kuwapigia kura zote wagombea wa CCM ili chama kipate ushindi wa kishindo kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.

Aliongeza kuwa kampeni zake zimejikita zaidi katika kuonesha mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia, huku akiahidi kuendeleza jitihada za kuimarisha huduma za kijamii, miundombinu na kuinua uchumi wa wananchi wa Jimbo la Mkuranga.

Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Kata ya Bupu, Mhandisi Abbas Msangule, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za Madala, vituo vya afya na zahanati katika Wilaya ya Mkuranga, akisisitiza kuwa miradi hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo.