Wachambuzi wataja sababu Tanzania kupaa maboresho ya utawala bora kidunia

Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya uongozi na utawala bora nchini wamesema mageuzi ya falsafa ya utawala yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto zilizokuwapo awamu ya tano, yamechangia kupanda viwango kwenye kipimo cha utawala bora duniani.

Kauli hiyo inakuja kufuatia ripoti ya Chandler Good Government Index (CGGI) 2025, iliyoonesha kuwa, Tanzania imeongoza kwa kasi ya ukuaji wa utawala bora barani Afrika, ikipanda kutoka nafasi ya 82 mwaka 2021 hadi nafasi ya 78 mwaka 2025 duniani na kushika nafasi ya sita kwa Afrika.

Akizungumzia mafanikio hayo leo Jumatatu Septemba 8, 2025 alipozungumza na Mwananchi kwa simu, Wakili wa Mahakama Kuu na mchambuzi wa siasa na utawala bora, Dk Onesmo Kyauke amesema kupanda kwa viwango hivyo kumetokana na jitihada za Serikali katika kuimarisha taasisi na huduma muhimu za kijamii.

“Utendaji bora wa taasisi za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano, pamoja na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati, ni miongoni mwa mambo yaliyosukuma Tanzania kupaa kwenye viwango vya utawala bora,” amesema Dk Kyauke.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema kupanda huko kumetokana na juhudi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita za kurejesha mifumo ya utawala bora kwa kuondoa changamoto zilizojitokeza katika awamu ya tano.

“Kipindi cha awamu ya tano kulikuwa na changamoto nyingi za kiutawala, lakini uongozi wa sasa umeweka dira na kuimarisha misingi ya utawala bora, hali iliyosaidia kupanda kwa viwango vya kimataifa,” amesema Dk Mbunda.

Amefafanua kuwa, viashiria vinavyotumika na CGGI vimegusa maeneo ambayo Serikali ya Tanzania imeyaboresha, ikiwamo uongozi na maono, sheria na sera madhubuti pamoja na kuimarika kwa soko.

CGGI hupima ufanisi wa Serikali za mataifa 120 duniani kupitia nguzo saba kuu za uongozi na maono ya mbeleni, sheria na sera madhubuti, taasisi imara, usimamizi wa fedha, soko lenye mvuto, nafasi na sifa kimataifa na kusaidia watu kupanda kimaisha.

Kwa mwaka 2025, ripoti hiyo imeonesha Tanzania ikiongoza kwa ukuaji wa utawala bora Afrika, ikifuatiwa na Rwanda.

Mauritius iliyoendelea kushika nafasi ya juu zaidi barani Afrika, imeshuka kidunia kutoka nafasi ya 36 mwaka 2021 hadi 51 mwaka 2025.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imeshika nafasi ya sita barani Afrika nyuma ya Mauritius, Rwanda, Botswana, Morocco na Afrika Kusini. Katika kumi bora za bara hilo, Tanzania inafuatiwa na Misri, Senegal, Ghana na Algeria.

Ripoti imebainisha kuwa, Tanzania imepanda nafasi kutokana na mageuzi ya kisera na kiutawala, ikiwamo utekelezaji wa Mradi wa Digital Tanzania na kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Data, hatua zilizoweka msingi wa utawala unaotumia teknolojia na kuongeza usalama wa kidijitali.

Aidha, imani ya kimataifa imeimarika kutokana na sera thabiti na uhusiano wa kidiplomasia, hali iliyoongeza uwekezaji wa mitaji kutoka nje. Takwimu zinaonesha uwekezaji wa ndani na nje uliongezeka kwa asilimia 21.6 na kufikia dola za Marekani bilioni 6.56 (takribani Sh16 trilioni) katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2024.

Ripoti hiyo pia imeonesha kuwa kati ya nchi 28 za Afrika zilizopimwa, Tanzania na Rwanda pekee ndizo zilizopanda katika viwango vya utawala bora kati ya mwaka 2021 na 2025.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Tanzania imeshuka kidogo katika vipengele vya taasisi imara na usimamizi wa fedha, huku maeneo mengine yakionesha kuimarika.