Watatu wajitosa urais TOC, yumo aliyekuwa mkurugenzi wa michezo

Wagombea  watatu wamejitosa  kuwania nafasi ya urais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kupitia uchaguzi utakaofanyika Oktoba 4, 2025 mjini Morogoro.

Wagombea hao ni  Leonard Thadeo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini.

Wengine ni makamu wa rais wa TOC anayemaliza muda, Henry Tandau na Nasra Juma Mohammed.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya uchaguzi huo, Ibrahim Mkwawa amesema katika nafasi ya makamu amejitokeza mgombea mmoja pekee, Suleiman Mahmoud Jabir.

Amesema katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu, wagombea 18 wamejitokeza, watatu wakichuana kuwania urais, mgombea mmoja katika nafasi ya makamu wa rais na wagombea 14 katika nafasi ya ujumbe.

Wagombea wa ujumbe waliojitokeza kwa upande wa Tanzania Bara ni Devotha Marwa, Fatma Yasoda, Muharami Mchume, Khalid Rushaka, Donald Massawe, Elias Mkongo, Noorelain Shariff na Suma Mwaitenda.

Upande wa Zanzibar waliojitokeza ni Mwatima Bakari Abdi, Suleiman Ame Khamis, Faida Salmin Juma, Makame Ali Machano, Juma Khamis Zaidy na Abdulrahman Said Simai.

Mkwawa amesema baada ya hatua ya uchukuaji na urejeshaji fomu, kesho Septemba 9-10, 2025 Kamisheni itaanza kupokea mapingamizi na Septemba 11-14 itayasikiliza kabla ya kutoa uamuzi Septemba 16.

“Septemba 18 itakuwa ni usaili kwa wagombea wa Tanzania Bara na Septemba 21 itakuwa ni kwa wagombea wa Zanzibar na siku inayofuata, tutatoa orodha ya mwisho ya wagombea.”

 Kampeni za uchaguzi huo zitaanza Septemba 24, zitafanyika kwa siku 10 hadi Oktoba 3 na Oktoba 4, ndipo wapiga kura watachagua Kamati ya Utendaji ya TOC katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mjini Morogoro.

Amesema katika nafasi ya ujumbe, wagombea watakaochaguliwa ni 10, nusu wakitoka Bara na nusu nyingine ni kutoka Zanzibar.

Katika uchaguzi huu, IOC (Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa italeta mtu ambaye atakuwa muangalizi wa kimataifa.