Yanga bab kubwa… Yatangaza kuipiga bao Al Ahly

WANACHAMA wa Yanga jana kwa kauli moja wamepitisha bajeti ya Sh 33 bilioni kwa msimu ujao, ikiwa ni zaidi ya Sh8 bilioni ukilinganisha na ile ya msimu uliopita ambao klabu hiyo ilitwaa mataji matano, huku uongozi ukiitangaza thamani ya klabu hiyo sasa ni Sh100 bilioni.

Thamani hiyo ni zaidi na ile iliyonayo Al Ahly ya Misri ambayo ndio inayoongoza orodha ya klabu zenye thamani kubwa Afrika ikiwa ni Euro 31 milioni (zaidi ya Sh90 bilioni), ikiziburuza klabu nyingine tisa maarufu barani humo.

Mkutano mkuu wa Yanga wa kufunga msimu wa 2024/25 na kufungua wa 2025/26 ulifanyika kwa kishindo ukishusha nondo muhimu.

Mkutano huo ulioanza saa 5:37 asubuhi kwenye Ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam ukitumia takribani saa nne, ulitawaliwa na amani na furaha ukihudhuriwa na wanachama 627 kutoka matawi 163 sambamba na viongozi mbalimbali walioalikwa mbali na wale wa klabu chini ya Injinia Hersi Said na Arafat Haji.

Akidi ya mkutano huo ilikamilika kwa wanachama hao 627 kutoka matawi 163 walihudhuria ikiwa ni ongezeko kutoka wanachama 496 wa mkutano mkuu kama huo uliopita.

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wanachama walikuwa wakiandikishwa kisha wanapiga uzi mpya wa klabu ili kuingia ndani ya ukumbi.

Wakati Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said akianza hotuba yake iliyotumia saa 1:56, kubwa lililobeba na kuufurahisha ukumbi wa mkutano ni hatma ya ujenzi wa uwanja. Eneo hilo awali ndiko ulikokuwa Uwanja wa Kaunda ulioifanya Yanga kuwa klabu ya kwanza kumiliki uwanja kabla ya mambo kuwatibukia na kuhaha kuurejesha, ila kikwazo ilikuwa eneo hilo kuwa dogo na kuchakarika kuiomba serikali iwaongezee na kufanikiwa hivi karibuni na kufikia ukubwa wa mita za mraba 37,500.

Akizungumza mbashara kwa njia ya simu katika mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Deo Ndejembi alisema wanatambua maombi ya klabu hiyo kwenye ongezeko la eneo hilo.

Ndejembi aliwatangazia wanachama wa Yanga kuwa ndani ya wiki mbili hati hiyo itakuwa imekamilika na itakabidhiwa kwa uongozi wa klabu hiyo.

“Nilipata heshima ya kukaribishwa kama Mwananchi mwenzenu, lakini kwa majukumu nimeshindwa kufika,” amesema Ndejembi na kuongeza;

“Kwanza niupongeze uongozi wa Yanga chini ya Rais Hersi, umekuwa mahiri sana kufuatilia mahitaji ya klabu. Kuna hati ambayo tulikuwa tunaishughulikia kwa karibu iweze kutoka niwaahidi ndani ya wiki mbili hizi tutakuwa tumeshaikamilisha na itatoka.”

Aidha, Hersi amemshukuru Ndejembi kwa kufanikisha hilo huku pia akiomba salamu zao njema zifikishwe kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha maombi yao.

Ndani ya hotuba ya Hersi amefichua kwamba wakati wa presha kubwa ya kutakiwa kuuzwa kwa mshambuliaji wa timu hiyo, Clement Mzize, klabu hiyo ilipokea ofa ya Dola 2 milioni.

Hersi alisema ofa ya mwisho iliyokuja klabuni ilikuwa Dola 2 milioni (zaidi ya Sh 5 bilioni).

Hersi alisema hata hivyo, uongozi ulizuia kumuuza, akifafanua isingekuwa rahisi kufanya biashara hiyo, kwa kuwa bado Yanga ilikuwa inahitaji nguvu ya mshambuliaji.

“Ofa zilikuwa nyingi sana kwa kijana wetu, lakini Yanga haikuwa na nia mbaya tulikuwa tunajua tunachokitaka,” alisema Hersi na kuongeza;

“Wakati wa presha wa hizo za ofa, Mzize alinipigia simu akaniuliza ‘rais wangu, niambie msimamo wa klabu ni upi, unataka niende au nisiende.’ Nikamwambia Mzize, tulia kwa sasa piga kazi na timu ya taifa, endelea kukiwasha piga mabao, ukimaliza CHAN tutazungumza.”

Hersi alisema, baada ya fainali hizo Mzize akaboreshewa masilahi na kuwa mchezaji anayelipwa vizuri ndani ya klabu hiyo.

“Hivi tunavyozungumza, Mzize amebakiza miaka miwili, akimaliza mwaka mmoja ujao hapo ndio tutaangalia namna ya kumuuza,” alisema Hersi bila kufafanua wapi, kwani katika dili za Mzize alitakiwa na Kaizer Chiefs, Al Masry na Esperance.

Yanga pia ilitangaza itatumia kiasi cha Sh33 bilioni kwa msimu ujao wa 2025-26 kuhakikisha inaendelea kutamba.

Akitangaza bajeti hiyo Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji alisema bajeti hiyo ni ongezeko la Sh8 bilioni kulinganisha na bajeti ya Sh25.3 bilioni ya msimu uliopita.

Arafat alisema katika bajeti ya msimu uliopita, Yanga ilibaki na kiasi cha Sh307 milioni kutoka kwenye vyanzo vyake vyote vya mapato.

Hata hivyo, Arafat alisema licha ya klabu yao kupanga kutumia kiasi hicho kwa msimu ujao bado watakabiliwa na upungufu wa sawa cha Sh12.9 bilioni kufikia bajeti yao hiyo.

“Kama mlivyoona vyanzo vyetu vya mapato tunatarajia kukusanya kiasi cha Sh 20,728,584,659 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato,” alisema Arafat na kuongeza;

“Kwa hiyo ndugu zangu wanachama bado tuna kazi ya kutafuta kiasi cha Sh12 bilioni ili kufanikisha bajeti yetu ya msimu ujao, tukifanikisha hilo tunaweza kujihakikishia mambo yetu kwenda sawa.”

Kocha wa Yanga, Romain Folz ni kama kashindikana katika ishu ya kucheka, kwani mapema jana asubuhi aligeuka gumzo katika mkutano mkuu wa klabu hiyo, baada ya kugoma kabisa kutabasamu kwenye majaribio mawili tofauti aliyofanyiwa na wanajangwani.

Iko hivi. Folz ametua na benchi la ufundi katika mkutano mkuu huo wakati wa utambulisho unaendelea ikafika hatua ya kutambulishwa kwa Mfaransa huyo.

Utambulisho huo ukafanywa na Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe ambapo akawaomba wajumbe wa mkutano mkuu kuhakikisha wanashangilia mpaka kocha huyo atabasamu kwa mara ya kwanza.

Kocha huyo hajawahi kuonekana akicheka wala kutabasamu katika picha zake tangu akiwa anafanya kazi Afrika Kusini na Kamwe alitaka kumlazimisha kiaina atabasamu, lakini alichomoa.

“Ndugu zangu wanachama, nawaletea jukumu hili nyie sisi tumeshindwa hebu leo nataka mpige makofi na kumshangilia mpaka atabasamu,” alisema Kamwe.

Hata hivyo, licha ya shangwe kubwa la wanachama lakini Folz aliishia kupiga makofi pekee akiwageukia wanachama hao.

Kamwe hakuishia hapo akawapa nafasi ya pili wanachama hao kujaribu tena kumshangilia kocha huyo akisimama, lakini bado Folz alishindwa kutabasamu.

Baada ya tukio hilo Kamwe akasema: “Wanachama na nyie pia mmeshindwa? Basi hiki chuma kitatabasamu Septemba 16, tutakaposhinda mchezo wetu.”

Katika Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Mfumo wa Uendeshaji wa Klabu ya Yanga, Alex Mgongolwa, alisema kwa sasa thamani ya timu hiyo imefikia kiasi cha Sh100 bilioni.

Thamani hiyo ni kubwa kuliko hata iliyo nayo klabu ya Al Ahly ambayo ni Euro 30 Milioni ambao ni zaidi ya Sh88 bilioni) ikiwa ni zaidi ya Sh12 bilioni na kuifanya Yanga sasa kuwa klabu yenye thamani kubwa zaidi barani Afrika kwa muktadha huyo uliotangazwa mkutanoni.

“Nichukue nafasi hii kuwaambia rasmi wanachama wa Yanga, thamani ya timu yetu imefikia Sh100 bilioni,” alisema Mgongolwa.

Hakuna ushahidi rasmi wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa Yanga ina thamani ya Sh100 bilioni kama ilivyotangazwa jana kwenye mkutano huo wa Yanga.

Hii ni kwa sababu hakuna ripoti rasmi, ya kibiashara au ya ufanisi, iliyotolewa na klabu au taasisi ya inayohusiana na kuthaminisha, inayosema thamani ya Yanga ni Sh100 bilioni.

Ripoti zilizopo zinaonyesha mapato (revenue) ya msimu 2023/24 ni takribani Tsh 21.2 bilioni, lakini klabu bado ilipata hasara ya Tsh 1.1 bilioni.

Kadhalika udhamini na mapato mengine kutoka kwa SportPesa yalikuwa ya Sh12.3 bilioni  kwa miaka mitatu iliyopita kabla ya hivi karibuni kusainiwa mkataba mpya wenye thamani ya Sh 21.7 bilioni) kwa miaka mitatu, mbali na wadhamini wengine, lakini ikiwa sio thamani ya klabu.

Thamani hiyo ni kubwa kuliko iliyonayo Al Ahly ya Misri ambayo ndio inayoongoza kwa mujibu wa taarifa rasmi ikiwa na thamani ya Euro 31 milioni (zaidi ya Sh 90 bilioni) ikiongoza klabu nyingine tisa kwa mujibu ya orodha ya mwaka jana..

Kwa hali halisi ilivyo ni kwamba klabu ya soka inapigwa thamani yake kwa mambo kadhaa ikiwamo haya manne ya msingi;

1. Enterprise Value (EV)- Hii ndio mbinu inayotumika na mashirika kama Forbes na Football Benchmark. EV inahesabiwa kwa kuongeza thamani ya usawa (equity) pamoja na deni neti. Kwa mfano, Real Madrid ina thamani ya takriban $6.6 bilioni, Manchester United $6.6 bilioni, na Barcelona $5.65 bilioni

2. Multiples ya Mapato (Revenue Multiples)- Njia hii inatumia mara nyingi kwenye klabu zinazopimwa kwa biashara. Thamani = Mapato ya Mwaka × Toleo la Soko (multiple), kwa kawaida kwa viwango vya juu hasa kwa klabu za juu za Ulaya.

3. Multivariate Models- Vipimo vingine vinachanganya vipimo vingine kama mapato, thamani ya wachezaji (player market value), thamani ya Uwanja (stadium) na ushawishi wa chapa (brand). Mfano mmoja ni “Markham multivariate model” unaochukua parameta kama uzalishaji, matumizi ya nguvu kazi, na utumiaji wa uwanja .

4. Majaribio ya Kiuchumi (Regression-based Models)- Makadirio ambayo yanachanganya takwimu tofauti kama mapato, thamani ya wachezaji, na idadi ya wafuatilia (followers) kutabiri thamani ya klabu, kama ilivyofanywa kwa klabu za Ulaya na Japani

Hersi alifafanua wajumbe wa mkutano huo juu ya muundo wa mfumo  wa uendeshaji wa klabu hiyo akisema nguvu kubwa ya Bodi itatoka klabuni kwao na sio wawekezaji.

Hersi alisema muundo huo, Bodi itaundwa baada ya mchakato wa mabadiliko kukamilika utakuwa na nguvu kwa wanachama ambao wenye Mali watamiliki asilimia 51 huku wawekezaji watagawana asilimia 49.

Wakati mkutano huo unakaribiwa kufungwa Yanga ikamtangaza msanii mkubwa ambaye atatumbuiza kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi Septemba 12. Alitajwa msanii wa lebo ya Wasafi, Zuchu kuwa atabeba shoo ya tamasha hilo akiwa pamoja na wasanii wengine wakali.