Singida. Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Dk Bashiru Ali, amevunja ukimya kwenye kampeni za mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, akieleza namna alivyopokea kijiti cha urais katika mazingira magumu lakini akalivusha Taifa salama.
Dk Bashiru ameeleza hayo leo Septemba 9, 2025 kwenye mkutano wa kampeni za Samia, wakati akijenga hoja kueleza kwa nini Watanzania wana kila sababu ya kumchagua mgombea huyo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Dk Bashiru amekuwa kimya kwa muda mrefu tangu alipofariki dunia kwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, ambaye ndiye alimteua kwa mara ya kwanza kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na baadaye akamteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021.
Akizungumza kwenye uwanja wa Bombadia mjini Singida, Dk Bashiru amesema alikuwa katibu wa vikao vya kamati kuu, hivyo anaelewa mazingira yaliyokuwepo, yanayomfanya kumwona Samia ni kiongozi bora, mtulivu na jasiri katika kazi zake.
Amesema wakati huo kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko -19, na muda mfupi baadaye Taifa likampoteza Rais aliyekuwa madarakani, jambo ambalo kwa mataifa mengine lingesababisha mgawanyiko, lakini Tanzania ilivuka salama chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Tulipoteza kiongozi jasiri aliyejua namna ya kukabiliana na ugonjwa huu, na hata baada ya kufariki, ule mpango na makakati yake ndio ulituvusha, na Mama Samia ndiye aliyepokea kijiti cha mkakati huo.
“Msiwe na mashaka, Watanzania wenzangu, huyu kiongozi wetu ana utulivu wa aina yake, ana ujasiri na umakini wa aina yake kwa sababu hali hiyo ilihitaji ujasiri na umakini. Sifa hiyo inatosha kumwongezea nafasi atuongoze,” amesema.
Mbali na kueleza uzoefu wake kwenye chama wakati huo, Dk Bashiru amesema alitoka huko akawa Katibu wa Baraza la Mawaziri akiwa Katibu Mkuu Kiongozi, nafasi iliyomfanya kushiriki katika vikao vya juu vya uamuzi.
“Nilishiriki katika vikao vya kutuvusha baada ya msiba… nawapa ushuhuda wa pili, kiongozi wetu huyu (Samia) alionesha umakini, utulivu na ujasiri mpaka tukavuka.
“Matukio hayo mawili yakitokea katika mataifa mengine, hasa katika nchi zetu zinazojijenga, huacha maafa makubwa, mataifa husambaratika. Leo Taifa letu sio tu lina amani, ni Taifa moja,” amesema Dk Bashiru huku akishangiliwa na wananchi.
Ameongeza kuwa msingi wa sifa hizo umetokana na uwezo wa CCM kuandaa viongozi, hivyo sifa hizo si zake, bali ni za chama kilichompa misimamo na yeye akaisimamia. Amesisitiza kwamba “ni mgombea bora wa urais wa chama bora.”
Ameongeza kuwa Samia amefanya kazi kubwa ya kulinda ubinadamu na heshima ya watu wake, kwani maskini na matajiri wakikosa huduma ya maji, wanakosa heshima na ubinadamu.
“CCM kinajenga shule, zahanati, vituo vya afya ili kulinda utu na heshima ya kila mtu nchini,” amesema Dk Bashiru, ambaye alieleza namna alivyoshiriki na kushuhudia kazi kubwa aliyoifanya alipokuwa serikalini kama Katibu Mkuu Kiongozi.
Mwanazuoni huyo amesema usawa wa wanaume na wanawake siyo suala la hiyari, bali ni lazima. Alisisitiza kwamba usawa wa binadamu ndiyo msingi wa amani, na usawa wa binadamu ndiyo msingi wa umoja wa Watanzania.
Akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea urais wa CCM, Samia, aliungana na Dk Bashiru na kusema wanafanya kazi ili kulinda utu wa binadamu kupitia huduma mbalimbali wanazozipeleka kwa wananchi kama vile maji, afya na elimu.
“Uwekezaji tunaoufanya ni kujali utu wa mtu. Tunataka kila tunachokifanya kijali utu wa mtu. Tunaomba tupeni ridhaa, tukaguse maisha ya kila Mtanzania,” amesema Samia.
Mgombea huyo wa urais ameahidi kuendelea kutafuta masoko ya mazao ya dengu, mbaazi na ufuta kwa ajili ya wakulima nchini, na hadi sasa mazungumzo na India kuhusu ununuzi wa mazao hayo yanaendelea.
Ahadi hiyo ya Samia ilitokana na ombi lililowasilishwa kwake na mgombea ubunge wa Ilongero, Haiderali Gulamali, aliyesema wakulima katika jimbo lake wamelima kwa wingi dengu lakini wamekosa masoko ya uhakika, hivyo alimtaka Samia aseme neno kuhusu wakulima hao.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Samia amesema wanaendelea kutafuta masoko ya mazao hayo ili kuwanusuru na kwamba watatoa vibali vya kuuza nje kwa wale wenye sifa hizo.
“Tunaendelea kutafuta masoko hasa ya dengu na mbaazi. Sasa tuko kwenye mazungumzo na India, changamoto ni kwamba nchi nyingi zimezalisha kwa wingi, hivyo mahitaji yamekuwa madogo.
“Niwahakikishie kwamba hatutashuka chini ya asilimia 60 ya bei ya soko la dunia,” amesema Samia, huku akiongeza kuwa pia watapitia mfumo wa ushirika nchini ili kuongeza tija kwa wakulima.
Samia amesema wanaendelea kuboresha mifumo ya usafirishaji wa mazao kwa kutumia teknolojia ambayo humkutanisha moja kwa moja msafirishaji na mkulima, bila kuingizwa mtu wa kati (dalali).
Wazungumzia kazi alizofanya
Aliyekuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema, kabla ya kutimkia CCM, Nusrat Hanje amesema wao kama vijana wako tayari kumtafutia kura Samia kwa sababu amefanya mengi katika mkoa huo na kuwaletea maendeleo.
Amesema katika miaka minne ya urais wake, Nusrat amesema amefanya kazi kubwa ya kuwajengea uwezo vijana kupitia mikopo inayotolewa na Serikali yake kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.
“Sisi watu wa Singida tumenyoosha maelezo kutokana na kazi kubwa alizofanya mgombea wetu. Ninaomba wote tukampigie kura Rais Samia ili akaendeleze kazi kubwa aliyoifanya,” amesema Nusrat.
Kwa upande wake, mbunge wa zamani, Lazaro Nyalandu amesema wametoka kwenye mchakato wa kura za maoni, sasa wanakuwa wamoja kuzitafuta kura za CCM, lengo ni kuonesha kwamba ni chama kilichokomaa.
Amesema Singida wameonja mazuri katika uongozi wa Samia, hivyo watasimama naye ili kuhakikisha wanamheshimisha.
“Nikuhakikishie, upendo wa Watanzania utadhihirika hapa Singida, tunakwenda kuhamasisha Watanzania wakupigie kura ili upate ushindi wa heshima,” amesema Nyalandu ambaye alitia nia katika jimbo la Ilongero lakini kura hazikutosha.
Mgombea ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Singida, Martha Mgwau amesema mambo aliyoyafanya katika miaka minne yamedhihirisha uimara wake na mapenzi kwa Watanzania hususani wananchi wa Singida.
Amesema Serikali yake imeboresha huduma za jamii hasa kwenye sekta ya afya kwani sasa vifo vya wanawake na watoto vimepungua kutokana na upatikanaji wa huduma bora na za uhakika kwa Watanzania wote.
“Ilani imesheheni mambo mema, imesheheni mambo ya kuwatumikia wananchi. Tuna imani na wewe, tunaamini unakwenda kutekeleza yote yaliyo kwenye ilani,” amesema.
Mgombea ubunge Jimbo la Iramba Mashariki, Jesca Kishoa amesema mambo ambayo Samia ameyafanya kwenye Taifa hili ya akieleza yenyewe huku akitoa mfano wa Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na daraja refu Afrika Mashariki.
Amesema watu wanaombeza sasa watakuwa wa kwanza kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Taifa hili, kwani wakati ukifika watajua na kuona.
Mgombea ubunge wa Singida Mjini, Yagi Kiaratu amempongeza Samia kwa kudumisha amani kwani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa hili.
Amesema miradi ya maendeleo imesambaa kila mahali, jambo ambalo halikuwahi kushuhudiwa miaka ya nyuma kabla yake.
“Singida tuna imani na wewe, chachu kubwa ni ilani uliyoiandika, watu wa Singida umewaambia unakwenda kujenga uwanja wa ndege, wanaachaje kukuchagua? Oktoba 29, 2025 tunakwenda kutiki kwa Mama Samia, kwangu na madiwani wa CCM,” amesema.
Mgombea ubunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba amesema Oktoba 29, 2025, Watanzania watakwenda kupiga kura kifua mbele kutokana na mambo uliyoyafanya ambapo mengine hayakuwahi kufanyika tangu uhuru.
Amesema Samia alipoingia madarakani, aliagiza kila tarafa ijengwe hospitali kubwa yenye hadhi ya wilaya, jambo ambalo amelitekeleza kikamilifu hasa katika jimbo lake la Iramba Magharibi.
“Kuna baadhi ya maeneo tangu uhuru hayakuwahi kuwa na barabara, leo barabara zinachimbwa kila mahali, maeneo mengi yanapitika. Nikuhakikishie, Oktoba 29, 2025 tunakwenda kukupigia kura uendeleze kazi uliyoianza,” amesema.
Mwenyekiti wa Wafugaji Tanzania, Mrida Mushota amesema mifugo ya Tanzania ilikuwa haiingii kwenye masoko ya kimataifa lakini Serikali ya Samia imetoa Sh69 bilioni kwa ajili ya kuchanja mifugo nchini ili iwe bora.
Amesema wafugaji wamejengewa majosho 754 nchi nzima, jambo ambalo limewatoa kwenye adha kubwa ya udumavu wa mifugo na hivyo kuwajengea ustawi katika kazi yao ya ufugaji.
“Umetufanyia kazi kubwa sisi wafugaji, tunaahidi kwenda kukupigia kura nyingi ili uendelee kutuletea maendeleo. Wafugaji tunakupenda na tunakuunga mkono katika kazi zako,” amesema kiongozi huyo wa wafugaji.
Makamu Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Mugeni Senge amesema machifu wanaendelea kumwombea ili awe na amani, afanye kazi zake kikamilifu katika kuwaletea wananchi maendeleo.
“Sisi tunakuahidi kura zote za Singida tutakupa wewe, wabunge na madiwani wa CCM,” amesema kiongozi huyo wa machifu ambaye amefikisha salamu za machifu kwenye mkutano huo.