Samia Aahidi Kongani ya Viwanda na Chuo cha Ufundi Ikungi – Global Publishers

Wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Ikungi Mashariki, wilayani Manyoni mkoani Singida, wamejitokeza kwa wingi leo Jumanne, Septemba 9, 2025, kushiriki mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akijinadi mbele ya mamia ya wananchi, Dkt. Samia aliahidi kuendeleza na kuongeza kasi ya miradi ya maendeleo ikiwemo kuanzisha kongani ya viwanda itakayoongeza thamani ya mazao na shughuli za kiuchumi ndani ya wilaya hiyo.

“Ndugu zangu kwenye ajira za vijana, awamu iliyopita tumefanikiwa kuleta kiwanda kimoja kikubwa, lakini tunajipanga kuja na kongani ya viwanda ndani ya wilaya hii, viwanda ambavyo vitaongeza thamani mazao yanayolimwa au shughuli zilizopo ndani ya wilaya hii,” alisema.

Aidha, Dkt. Samia alisisitiza kuwa wilaya ya Ikungi imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa nishati ya umeme, ambapo vijiji vyote 101 tayari vimeunganishwa na umeme, huku kazi ikiendelea kwenye vitongoji.

“Mbele tunakokwenda, mkitupa ridhaa, tunakwenda kumaliza kazi yote Tanzania nzima kila mtu awe na umeme,” aliongeza.

Kwenye sekta ya elimu, Dkt. Samia ameahidi kuendeleza sera ya elimu bure sambamba na kuongeza miundombinu ya madarasa ya shule za msingi na sekondari wilayani humo. Pia alitangaza mpango wa serikali ya CCM wa kujenga chuo cha ufundi ndani ya wilaya ya Ikungi ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa moja kwa moja utakaowaingiza kwenye ajira.

Mkutano huo ni sehemu ya kampeni za CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo Dkt. Samia anawania kuendelea kuongoza Tanzania kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.