Moshi. Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo amesema endapo atashinda nafasi hiyo ya ubunge, atahakikisha mradi wa stendi ya kimataifa ya mabasi Ngangamfumuni iliyokwama kwa zaidi ya miaka minne, inakamilika ndani ya muda mfupi.
Ujenzi wa stendi hiyo ambayo ilikumbwa na changamoto ya maji kuibuka chini ya ardhi, ulianza mwaka 2019 na ulitarajia kugharimu zaidi ya Sh17 bilioni hadi kukamilika kwake.
Shayo ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Mandela, vilivyopo Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
Aidha, Shayo ameeleza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha mradi huo muhimu wa usafirishaji unakamilika, akisema anajua njia za kufikia Serikali Kuu na yupo tayari kupigania stendi hiyo hadi ikamilike na iwe ni ya kihistoria mjini Moshi.
“Ndugu zangu imekuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu sana kupata nafasi ya kuwatumikia wananchi wenzangu wa Moshi, leo nasimama mbele yenu kama mgombea ubunge wa Moshi mjini nikiwa na moto wa uwajibikaji, utu, uwazi, uadilifu na uaminifu mkubwa mno,” amesema na kuongeza:
“Endapo mtanipa kura zote za kishindo nitashirikiana na Serikali kuhakikisha stendi ya Ngangamfumuni inakuwa ni stendi ya kihistoria hapa Moshi…
“Najua kujipenyeza ni moja kwa moja mpaka kwa mama kubisha hodi, (namwambia) wananchi wanataka stendi, naamini tutakuwa tumemaliza ndani ya miaka miwili au mitatu.”
Kuhusu changamoto ya barabara, Shayo amesema baadhi ya barabara za Moshi zilizojengwa kwa kiwango cha lami ni mbovu, hivyo endapo atakuwa mbunge atahakikisha barabara hizo zinafanyiwa matengenezo ya kutosha.
“Barabara nyingi za Moshi mjini hapa najua ni mbovu, zipo zilizowekwa lami lakini nyingine zina shida, Moshi ina lami katikati lakini pembezoni haifai, nipeni kura zote naenda kujipenyeza kuhakikisha tunatatua tatizo hili la barabara,” amesema Shayo.
Changamoto nyingine, ambayo amesema ataishughulikia, ni suala la taka akisema imekuwa ni changamoto kubwa magari ya taka kupita mtaani hivyo akaahidi kushirikiana na mamlaka husika kukubiliana na tatizo hilo.
“Takataka ni shida kubwa kutoa mtaani, na nyie mnajua nipeni kura zote, mpeni Rais Samia Suluhu Hassan kura zote ninaenda kushirikiana na madiwani wenzangu, mkurugenzi, Serikali Kuu gari za taka zitakuwa mpya na sio takataka,” amesema mgombea ubunge huyo.
Amesema kwa kuwa yeye anaishi Moshi na biashara zake anafanya hapo tangu mwaka 1994, anaifahamu na changamoto zake.
Pamoja na mambo mengine, amesema atahakikisha kunakuwepo na mahusiano mazuri baina ya ofisi ya mbunge na wananchi, ili aweze kuwasikiliza na kutatua changamoto zao kwa wepesi.
Aidha, Shayo ameahidi pia kushughulikia suala lililoshindikana muda mrefu la Manispaa ya Moshi kupandishwa hadhi na kuwa jiji, ili kuendelea kuchochea ukuaji wa maendeleo.
“Huu mfupa umewashinda watu wengi, ukiangalia Tanga ni jiji, Arusha ni jiji lakini Moshi siyo jiji, nitakwenda kukaa na mbunge wa Moshi Vijijini nitengeneze hoja ya upanuzi wa huu mji, haiwezekani wageni wanakuja kutoka ulaya kwa ajili ya utalii halafu wanashuka manispaa, sasa tunataka wakija washukie katika Jiji la Moshi.”
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, kwenda kuwapigia kura wabunge wote wa mkoa huo na mgombea urais wa CCM ili aweze kuongoza nchi kwa kipindi kingine cha pili.
“Niwaombe wananchi wote wa Moshi mjini tujitokeze kupiga kura, tukamchague Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na ndugu yangu Ibrahim Shayo kwa kura zote za ndio,” amesema Profesa Mkenda.