WAZIRI KOMBO AINADI DIRA YA ZANZIBAR KUWA KITOVU BORA CHA KIFEDHA AFRIKA MASHARIKI JIJINI LONDON

::::::::

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameinadi dira ya Tanzania ya kuifanya Zanzibar kuwa kitovu bora cha kifedha Afrika Mashariki. 

Balozi Kombo amewasilisha dira hiyo aliposhiriki mjadala uliyofanyika katika jengo la kihistoria la Guildhall jijini London chini ya kauli mbiu ya “Kuibua Zanzibar Kama Kitovu Bora cha Fedha Afrika Mashariki.” na kukutanisha viongozi kutoka katika sekta ya fedha, watunga sera, wawekezaji na wataalamu kutoka Uingereza na mataifa mengine. 

Mjadala huo uliandaliwa na Alderman Profesa Emma Edhem kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ukiongozwa na Mhe. Mbelwa Kairuki. 

Akizungumza kufungua mjadala huo, Mhe. Waziri Kombo alisisitiza kuwa Zanzibar ipo kwenye safari ya mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayolenga kuibua uchumi, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa kwa wananchi kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa lango la fedha za kimataifa, kituo cha kuaminika cha usuluhishi na mahakama ya kibiashara, pamoja na jukwaa la ubunifu katika sekta ya kifedha. 

“Zanzibar ipo kwenye safari ya mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayolenga kuibua uchumi, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa kwa wananchi. Dhamira ni kuifanya Zanzibar kuwa lango la fedha za kimataifa, kituo cha kuaminika cha usuluhishi na mahakama ya kibiashara, pamoja na jukwaa la ubunifu katika sekta ya kifedha,” alisema.

Waziri Kombo alibainisha kuwa Zanzibar ipo katika makutano ya Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, huku

ikiwa na uthabiti wa kisiasa na uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu, bandari, nishati na mifumo ya kidijitali. Alisisitiza kuwa uwazi, utawala bora na kufuata viwango vya kimataifa ndizo nguzo za kuimarisha imani ya wawekezaji.

Alieleza kuwa uanzishwaji wa kitovu hicho cha kifedha utaleta manufaa makubwa katika sekta za utalii,

nishati, uchumi wa buluu, viwanda na huduma za kidijitali. Pia utazalisha ajira, kukuza ubunifu kwa kushirikiana na vyuo vikuu na taasisi za utafiti, sambamba na kuimarisha mazingira salama ya usuluhishi wa kibiashara.

Waziri Kombo alitoa wito wa ushirikiano katika nyanja za fedha, sera, sheria, ujenzi, miundombinu na teknolojia ili kujenga mfumo wa ushindani na thabiti na kuwaalika wawekezaji, wabunifu na wataalamu kushirikisha maarifa na rasilimali kufanikisha dira hiyo kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kimataifa.

“Mjadala huu ni hatua muhimu ya kubadilishana mitazamo na kuimarisha ushirikiano wa kudumu. Pamoja, tunaweza kuibadilisha Zanzibar kuwa ishara ya ubunifu, uimara na fursa kwa Afrika na dunia nzima.” alisema Waziri Kombo.