Ahadi za vyama, ZEC ziwe kwa vitendo zaidi

Hivi karibuni, jumla ya vyama 18 vya siasa vilitia saini hati ya makubaliano ya kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Zanzibar unafanyika kwa amani, uwazi na kwa misingi ya kidemokrasia. Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji George Kazi, yamelenga kujenga mazingira bora ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyia Jumatano Oktoba 29, 2025.Hata hivyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakikushiriki katika hatua hiyo, jambo linaloibua maswali kama ilivyokuwa kwa upande wa Bara. Hatua ya vyama vingine 18 kushirikiana inachukuliwa kama mfano wa ustaarabu na dhamira ya kulinda amani wakati wa uchaguzi.Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vyama vinatakiwa kuendesha kampeni kwa lugha za kistaarabu, kuepuka vitisho, uchochezi, matusi na kauli zinazoweza kuchochea chuki.Lakini historia ya chaguzi zilizopita inaonyesha kuwa mara nyingi makubaliano haya hayatekelezwi ipasavyo.Kumekuwapo na malalamiko kwamba baadhi ya viongozi wa serikali hususani ngazi za chini kama mitaa na shehia huwarubuni wananchi ili wakipigie kura chama wakitakacho jambo ambalo ni kinyume na sheria.Kauli hiyo ilisambaa mitandaoni lakini ZEC wala Ofisi ya Msajili wa Vyama haijaitolea kauli ya kulaani.Changamoto nyingine ni matumizi ya vyombo vya habari vya serikali huku Zanzibar ambavyo vinadaiwa kutotimiza wajibu wa kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote.Kwa sasa, taarifa zinazomsifu mgombea wa CCM zinapewa kipaumbele, huku hata vipindi vya burudani vikigeuzwa kuwa jukwaa la kampeni. Kwa mtazamo wa baadhi ya wananchi, hali hii ni dhihirisho la upendeleo ambao unakiuka misingi ya vyombo vya habari vya umma vinavyofadhiliwa na kodi za wananchi wote, si chama kimoja pekee.Wachambuzi wanasema ZEC yenyewe inakabiliwa na changamoto ya kuaminika. Katika chaguzi zilizopita, wagombea wa upinzani zaidi ya 10 walienguliwa kwa madai ya kukosa sifa, wakiwamo wanasiasa waliowahi kushika nafasi kubwa serikalini.Hata marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na kiongozi mashuhuri wa upinzani, hakusalimika na mizengwe ya aina hiyo.Hali hiyo kama hii kama isipodhibitiwa, inaweza kuwapa upendeleo wagombea wa CCM kupita bila kupingwa na ikasababisha kuzua maswali iwapo kweli ni CCM pekee inayoweza kutoa wagombea “wanaostahili” huku wapinzani wakikosa sifa.Wananchi wanasubiri kuona kama ZEC chini ya Jaji Kazi itajirekebisha na kusimamia haki au itarudia makosa ya nyuma.Malalamiko mengine ni kuhusu kura za mapema, ambazo baadhi ya vyama vya upinzani hudai kuwa ni chanzo cha kupenyezwa kura bandia.Wapinzani wanasema mfumo huo ndio uliosababisha machafuko katika chaguzi zilizopita. Ili kuepusha hali kama hiyo, ZEC inapaswa kuwa wazi kwa kueleza idadi kamili ya wapiga kura watakaoshiriki mapema na kuhakikisha kura hizo zinahesabiwa kwa utaratibu maalum tofauti na kura za siku ya uchaguzi.Hali ya kisiasa visiwani pia inakumbwa na changamoto ya maandiko ya matusi na uchochezi katika maeneo ya wazi.Pamoja na maeneo hayo kujulikana, wahusika mara nyingi hawaadhibiwi. Wakati huo huo, polisi wamekuwa wakilalamikiwa kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya vurugu, ikiwamo vizuizi vya barabarani vinavyowekwa na makundi ya watu wakati wa misafara ya wapinzani. Mara nyingi hali hizo huishia kwa vurugu, majeruhi, risasi za moto au mabomu ya machozi.Kwa mujibu wa wachambuzi, iwapo vitendo hivi havitadhibitiwa kisheria, havitazua tu taharuki bali pia vitaathiri taswira ya uchaguzi wa Zanzibar mbele ya macho ya dunia.Ili kuabiliana na hili, nivikumbushe hata vyama vyenyewe wajibu wao wa kuhakikisha hotuba za kampeni zinajenga mshikamano badala ya kuibua chuki.Viongozi wanaopanda majukwaani wanapaswa kutumia lugha zenye staha na kuhimiza mshikamano wa kitaifa. Hii ndiyo dhamira ya msingi ya makubaliano yaliyosainiwa, lakini utekelezaji wake ndiyo kipimo kikuu.Zanzibar iko katika kipindi nyeti kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba. Makubaliano ya vyama 18 vya siasa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi wa amani na wa haki.Lakini changamoto zilizobainishwa, matumizi mabaya ya vyombo vya dola, upendeleo wa vyombo vya habari, mizengwe ya wagombea kuenguliwa, kura za mapema na vitendo vya uchochezi, vinaweza kuharibu mchakato huu.Ni wajibu wa ZEC sasa kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa uwazi na wa haki kwa vitendo na si kwa maneno pekee. Polisi nao wanapaswa kuwa walinzi wa kweli wa amani badala ya kutumiwa kama silaha za kisiasa.Vivyo hivyo, vyama vyote vinapaswa kuonyesha mfano wa kisiasa kwa kuendesha kampeni za kistaarabu.Ikiwa makubaliano haya yatatekelezwa ipasavyo, basi Zanzibar inaweza kufanikisha uchaguzi wa kidemokrasia unaokubalika na pande zote. Lakini iwapo historia ya nyuma itajirudia, makubaliano haya hayatakuwa na maana.