Aliyekuwa Waziri Mkuu Thailand kutupwa jela mwaka mmoja

Bangkok. Mahakama Kuu ya Thailand imeamuru waziri mkuu wa zamani, Thaksin Shinawatra, kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, baada ya kubaini hakutimiza ipasavyo kifungo chake cha awali alichotumia muda mwingi hospitalini badala ya gerezani.

Katika uamuzi uliosomwa juzi Jumatatu, majaji walisema Thaksin, mwenye umri wa miaka 76, alihamishiwa hospitalini kinyume cha sheria wakati akianza kutumikia kifungo chake mwaka 2023.

“Kumpeleka hospitalini haikuwa halali. Mshtakiwa alijua ugonjwa wake haukuwa wa dharura, hivyo muda aliotumia hospitalini hauwezi kuhesabiwa kama kifungo cha jela,” inasomeka sehemu ya hukumu hiyo.

Mahakama ilitoa hati ya kumpeleka moja kwa moja Gereza Kuu la Bangkok kuanza kutumikia kifungo hicho.

Thaksin, bilionea na mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa, alitumia sehemu kubwa ya kifungo chake cha awali katika chumba cha hospitali na hakuwahi kulala hata usiku mmoja  selo, jambo lililoibua ghadhabu na shaka miongoni mwa wananchi waliodai upendeleo wa kisheria.

Mahakama iliongeza kuwa, Thaksin kwa makusudi alichelewesha muda wa kuondoka hospitalini ili kuepuka kifungo cha kweli gerezani.

Safari ya kisiasa yenye utata

Thaksin alikuwa uhamishoni kwa zaidi ya miaka 15 baada ya kupinduliwa madarakani na jeshi mwaka 2006. Alirejea Thailand mwaka 2023 akikabiliwa na hukumu ya miaka minane jela kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Hata hivyo, kifungo hicho kilipunguzwa na Mfalme Maha Vajiralongkorn hadi mwaka mmoja, na baadaye alipewa msamaha wa muda baada ya kutumia miezi sita hospitalini.

Baada ya uamuzi huo, binti yake na mrithi wa kisiasa, Paetongtarn Shinawatra ambaye pia aliwahi kushika wadhifa wa waziri mkuu amesema baba yake bado ni kiongozi wa kiroho licha ya hukumu hiyo.

 “Baba yangu anaendelea kuwa kiongozi wa kiroho kutokana na mchango wake kwa Taifa na dhamira yake ya dhati kuboresha maisha ya watu,” amesema Paetongtarn mbele ya waandishi wa habari nje ya Mahakama.

Wafuasi wake wachache walikusanyika nje ya Mahakama Kuu wakimpa sapoti, huku ulinzi mkali ukiwekwa na polisi kuzuia vurugu.

Imeandaliwa na Mintanga Hunda kwa msaada wa mashirika ya habari