Azam yafanya mabadiliko, Father apewa urais, Popat makamu wake

Azam FC imetangaza mabadiliko ya muundo wa uongozi wake ambayo yanaanza msimu huu.

Mabadiliko hayo ni ya muundo wa kiutawala ambapo hivi sasa itakuwa inaongozwa na Rais wa Klabu na sio mwenyekiti.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 9, 2025 na Azam FC, aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Nassor Idrissa ‘Father’ sasa ndiye atakuwa Rais.

Wakati huohuo, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Nurdin Amin ‘Popat’ amepanda cheo na sasa anakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.    

“Bodi ya Azam Football Club imefanya mabadiliko ya kimuundo na mfumo wa klabu yanayoanza mara moja. Mabadiliko hayo yanahusu nafasi za juu za utendaji katika utawala.

“Nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu inabadilika na kuwa Rais wa Klabu (Club President). Hata hivyo, mtendaji wa nafasi hiyo anabaki kuwa Nassor Idrissa maarufu kama Father.

“Rais wa klabu atakuwa na makamu wawili: i. Makamu wa Rais anayeshughulika na timu kubwa (Vice President – Senior Team). Nafasi hii itashikwa na Abdulkarim Nurdin maarufu kama Popat. ii. Makamu wa Rais anayeshughulika na akademi (Vice President – Academy). Nafasi hii itashikwa na Omary Kuwe.

“Kutokana na mabadiliko haya, nafasi ya Mtendaji Mkuu (CEO) itajazwa baadaye. Kwa sasa, Abdulkarim Nurdin, ataikaimu hadi atakapopatikana mtendaji mwingine. Aidha, Mkurugenzi wa Fedha, Abdulkarim Shermohamed maarufu kama Karim Mapesa, ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi,” imefafanua taarifa ya Azam FC.

Ikumbukwe Nassor Idrissa alianza kuwa Mwenyekiti wa Azam FC kuanzia Januari 19, 2021 akichukua nafasi ya Shani Christoms.

Kabla ya uteuzi huo mwaka 2021, Father alikuwa akihudumu kama mkurugenzi mshauri wa klabu.

Kwa upande wa Popat, ameitumikia nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Azam FC kwa miaka saba tangu alipoteuliwa mwaka 2018.