Dodoma. Kampeni za kuwania nafasi ya urais, ubunge na udiwani, zimetimiza siku 10 tangu zilipozinduliwa Agosti 28, 2025, huku wagombea wa urais wa vyama mbalimbali wakizunguka huku na kule kunadi sera na kuzisaka kura.
Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameshafanya ziara katika mikoa saba kuomba kura, akianzia Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.
Kwa upande wa mgombea wa nafasi hiyo kwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu tayari pamoja na mgombea mwenza wake, Devotha Minja wametembelea mikoa mitano ndani ya siku hizo.
Katika kampeni hizo, Samia amejipambanua kwa mambo nane, huku mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi naye akiendelea kuchanja mbuga katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Mapokezi kwa mgombea urais kupitia chama hicho yamekuwa makubwa, wananchi wakijitokeza kwa wingi kusikiliza hoja na ahadi zake.
Chama hicho kimejipanga. Katika baadhi ya maeneo kimekuwa kikitoa usafiri kwa wanachama wa vijiji vya jirani kuwafikisha kwenye mikutano ya hadhara, jambo ambalo mgombea huyo amefafanua kuwa ni kuwasaidia wananchi hao kufika kwenye mikutano bila usumbufu.
“Kuna baadhi ya watu wanasema CCM kinabeba watu kwenye mikutano yake. Kwani kuna tatizo gani chama kikitoa magari kuwasaidia usafiri wanachama wake? Kwetu sio aibu kubeba watu kwenye magari kuwaleta kwenye mikutano, ili mradi hatuwatoi watu kutoka wilaya nyingine, wanatoka hapa hapa jirani,” alisema Samia.
Mwananchi imeshuhudia mwitikio chanya wa wanaCCM na wananchi wengine kuhudhuria mikutano hiyo huku wakivutiwa na ahadi zinazotolewa na mgombea huyo katika jamii yao.
Mkazi wa Mvomero, Sabas Kimweri alisema amefurahishwa na ahadi ya Samia ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo kwani limekuwa ni tatizo sugu linalowasumbua wakazi wa wilaya hiyo.
“Nimekuwa hapa kumsikiliza mgombea huyu anasema nini kuhusu Mvomero yetu. Nashukuru amegusia suala la maji, naamini atafanyia kazi jambo hilo ili nasi tupate huduma ya maji ya uhakika,” alisema mwananchi huyo, mkazi wa Mvomero.
Akiwa Mvomero mkoani Morogoro, Samia aliwaomba wananchi wakichague chama hicho ili kikaongoze utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Dira ya Taifa inatuelekeza kwamba ifikapo mwaka 2050 tuwe tumefikia kiwango cha uchumi wa kati wa juu, Tanzania ambayo uchumi wake itasimama, hatutategemea mikopo mikubwa.
“Na maandalizi ya kufika huko yanaanza kwenye miaka mitano ijayo, kwa hiyo niwaombe Oktoba 29, 2050 twende wote tukakipigie kura Chama cha Mapinduzi. Mkawapigie kura wabunge wenu na madiwani wenu ili waje wafanye kazi inayotakiwa,” amesema.
Mgombea huyo ameahidi kwamba wakichaguliwa tena watakamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha Dakawa na Njeula, pamoja na kuanza utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.
Pia, amesema watajenga kituo cha kupoza umeme Mvomero, chenye msongo wa kilovoti 220, ambacho kitakuwa kinasafirisha umeme kati ya Morogoro na Dumila.
“Niwaombe wananchi, tusimame pamoja kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi ili tuendelee kuwaletea maendeleo,” amesema Rais Samia huku wananchi waliohudhuria mkutano huo wakimshangilia.
Akiwa Tunduma, mgombea huyo aliahidi kumaliza tatizo la msongamano wa magari katika mji wa Tunduma kupitia mradi wa upanuzi wa barabara ya Tanzam.
Mji wa Tunduma unakabiliwa na changamoto ya msongamano wa magari unaosababishwa na malori ya mizigo yanayoelekea Zambia, jambo ambalo limekuwa likitatiza shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii katika mji huo maarufu kwa biashara.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni, Samia alibainisha mikakati ya kumaliza foleni hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tunduma – Igawa, kilomita 75.
Alisema baada ya maboresho makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kiwango mizigo kilinachopokelewa kimeongezeka kutoka tani milioni 15.8 kabla ya maboresho hayo, hadi kufikia tani milioni 28 zinazopokelewa sasa.
Alisema kiwango cha mzigo unaopita Tunduma pia kimeongezeka kutoka tani milioni 3.7 hadi tani milioni tisa, jambo linalosababisha msongamano wa malori katika mji huo unaopakana na Zambia.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, ameahidi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Tanzam kwa njia nne ili kumaliza tatizo hilo linalokwamisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Mgombea huyo wa urais ameeleza kwamba Serikali imeanza kukarabati reli ya Tazara ili kuiongezea uwezo wa kusafirisha mizigo kwenda Zambia, jambo ambalo litasaidia kupunguza malori ya mizigo katika mji wa Tunduma.
Kwa upande wa umeme, alisema watajenga kituo cha kupoza umeme cha kilovolti 730 ambapo kilovolti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa na kilovolti 330 zitauzwa nchi jirani ya Zambia.
Katika hatua nyingine, alisema Serikali ya Tanzania inafanya mazungumzo na mamlaka za Zambia ili kuzishawishi nazo kufanya kazi kwa saa 24 kama ilivyo upande wa Tanzania.
Huko Mbalizi mkoani Mbeya, Samia aliahidi kwamba Serikali yake itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima nchini huku akiwataka wajisakili kwani uwezo wa kutoa ruzuku hizo bado upo.
Katika maeneo yote aliyopita, mgombea huyo amekuwa akitoa ahadi kwa wananchi zinazolenga kuchochea maendeleo na ustawi wao hasa katika huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi.
Samia aliahidi kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwani matokeo ya ruzuku hizo yamekuwa ni makubwa hususani kwa Mkoa wa Mbeya ambako wanazalisha zaidi mazao ya pareto, mahindi, mpunga na maparachichi na asilimia 85 ya wananchi wake ni wakulima.
Amewahakikishia kwamba uwezo wa Serikali kutoa ruzuku bado upo, hivyo amewataka wajisajili na kutunza namba za siri huku akionya kwamba mbolea za ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa CCM, kwa upande wa Chaumma, kimeshafanya ziara katika mikoa mitano, kikiweka msisitizo wa kufanya maboresho katika maeneo makuu manane serikalini.
Mgombea urais kupitia chama hicho ni Salum Mwalimu, huku mgombea mwenza ni Devotha Minja, tayari kwa nyakati tofauti, wametembelea mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma na Morogoro.
Maeneo waliyoahidi mabadiliko ni suala la kodi, afya, kilimo, makazi bora, viwanda, maji safi, chakula na ustawi wa wakulima na wafugaji.
Akiwa Arusha, Mwalimu alijipambanua kama kiongozi anayeielewa Tanzania ya watu wa kawaida.
Katika mikutano ya kampeni iliyofanyika Makuyuni, Kwa Mromboo na Monduli, alisisitiza dhamira yake ya kutetea haki za wafugaji kwa kuondoa vikwazo vya malisho ya mifugo na kuwapa maeneo maalum yasiyovamiwa na wawekezaji wakubwa au hifadhi za wanyama.
Alitoa ahadi ya mageuzi makubwa katika sekta ya utalii, akisema serikali yake itapunguza masharti kandamizi kwa wazawa wanaotaka kushiriki katika biashara hiyo.
Aliahidi kwamba hata mmiliki wa pikipiki ataweza kutoa huduma za utalii na baadaye kuhitimu kupata leseni kamili.
Katika mkoa wa Kilimanjaro, Mwalimu alieleza azma ya kuijenga Moshi kama kituo cha biashara cha kimataifa kwa kujenga soko la kisasa la Kiboroloni, lenye hadhi ya Kariakoo, kwa lengo la kuhamasisha biashara ya mipakani na kupunguza msongamano wa watumiaji wa soko la Dar es Salaam.
Mkutano wa kampeni uliofanyika Kaanda. Hai Mashariki, alitangaza mpango wa kujenga bandari kavu Chekeleni, yenye miundombinu ya kuhifadhi mazao kama parachichi, vitunguu na ndizi, huku akiahidi fidia halali kwa watakaopisha ujenzi huo.
Mwalimu pia alisisitiza umuhimu wa SGR (reli ya kisasa)kuunganisha Kilimanjaro na Arusha ili kukuza biashara ndogo na sekta ya utalii.
Katika mkoa wa Tanga, Mwalimu alijikita katika uwezeshaji wa vijana kiuchumi, akiahidi kuondoa urasimu kwenye utoaji wa mikopo ya halmashauri na kuhakikisha kuwa sera za biashara zinawanufaisha wazawa.
Katika eneo la viwanda, Mwalimu aliahidi kuifanya Tanga na Morogoro kuwa kitovu cha viwanda vya Afrika Mashariki, kwa kufufua viwanda vya mkonge, mafuta na matunda. Alieleza kuwa kujengwa kwa kiwanda cha kusafisha mafuta Tanga kutapunguza bei ya mafuta kwa Watanzania.
walimu hakusita kuelezea ajenda yake yakuijenga Tanzania ya maziwa na asali akisisitiza kwamba rasilimali za taifa lazima zinufaishe kila Mtanzania, si kikundi kidogo cha watu wachache. Kwa upande wa Devotha, kwa siku nane tangu Septemba Mosi hadi 8 katika mikoa miwili ya Morogoro na Dodoma ameinadi chama hicho kwa mambo sita.
Jambo la kwanza aliloahidi katika mikoa hiyo miwili, ni chama hicho kufuta utitiri wa kodi kwa wafanyabiashara na wakulima kwenye mazao. Mbali na hayo chama hicho ikiuzingatia mkoa wa Morogoro kuweka nguvu zaidi kwenye kilimo cha miwa, Devotha amesema chama chake kitaimarisha kilimo cha miwa ili kukabiliana na uhaba wa sukari ambao mara kwa mara umekuwa ukitokea nchini. Mgombea mwenza huyo, amesema hakuna haja ya wananchi kuteseka na kununua sukari hadi Sh7000 wakati vipo viwanda vingi vya sukari lakini hakuna nguvu inayowekwa kwenye kilimo.
Agenda nyingine ya Chaumma, ni kukabiliana na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji,akiahidi upatikanaji wa kutosha maeneo ya kilimo na malisho. “Kule ambapo watu wanahodhi maeneo makubwa ya ardhi Chaumma tutarejesha kwa wananchi, nitamshauri Rais tushughulikie huu upungufu wa ardhi, kila mkulima na mfungaji wapate ardhi ya kutosha,” amesema.
Kero ya maji nayo iliibuliwa na chama hicho kama agenda muhimu kwa wananchi,Mgombea mwenza huyo amesema wapo wananchi wanaugua kutokana na kunywa maji machafu. Kupitia mpango huo Devotha ameahidi bili ya maji kwa mwezi haitazidi Sh1,000 kwani huduma hiyo ni muhimu kwa wananchi. Kwenye huduma za afya, Minja amesema haiwezekani wajawazito kwenda hospitali na vifaa vya kujifungulia pamoja na maji kwa ajili ya usafiri huku dawa zikiuzwa kwa bei kubwa.
“Kinachofanya dawa kuwa ghali ni kodi, unaponunua dawa ndani kuna kodi, kodi ikiondolewa gharama inakuwa chini, kwa dawa zinazotibu wananchi wengi Serikali zitatolewa bure gharama zitabebwa na Serikali”amesema.
Ameahidi kuwa Chaumma ukiwa ni mpango wa kuboresha sekta ya afya wananchi watapatiwa bima ambayo itawahudumia watu wote, akifafanua kuwa ndani ya bima hiyo kutakuwa na kifurushi cha chakula na kila mgonjwa anapofika hospitali lazima apate chakula.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mkazi wa Ngerengere, Ramadhani Salum maarufu kichoroko, akisema wanapokwenda hospitali kwa ajili ya matibabu hushauriwa na wataalamu kuwahi mitishamba kutokana na kutokuwapo dawa. “Ukienda hospitali unaambiwa mzee jipange hakuna dawa za kutosha, jambo la pili tunakunywa maji chumvi hadi tunapata henia,” amesema. Ahadi nyingine aliyoitoa Minja kwa Watanzania akiwa mkoani Dodoma, amesema endapo Chaumma kitashika dola ni kubinafsisha sekta ya nyumba ili wananchi wa vijijini wajengewe makazi bora na Serikali kupitia sekta binafsi.
Makazi hayo wananchi watalipa kwa kipindi cha miaka 50 kidogo kidogo na gharama za vifaa vya ujenzi vitashushwa kupitia kuondolewa kwa kodi kwenye vifaa vya ujenzi.
Kwa mkoa wa Dodoma pekee ameahidi kuufanya kuwa wa kijani kupitia kilimo na upatikanaji wa kutosha wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.