Darasa la saba waanza mtihani leo

Kibaha. Wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Kambarage Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani wameelezea namna walivyojiandaa na mtihani wa kuhitimu elimu hiyo unaotarajia kufanyika kwa siku mbili leo na kesho  nchini kote.

Wahitimu hao walioanza safari ya kusaka elimu tangu mwaka 2019 wanahitimisha hatua hiyo ikiwa ni maandalizi ya kuanza elimu ya sekondari mwakani.

Wakizungumza leo Jumatano Septemba 10, 2025 wakiwa shuleni hapo wamesema wanaamini watafanya vizuri kwa kuwa siku zote mitihani inatokana na masomo waliyofundishwa na walimu wao darasani.

“Sina wasiwasi naamini nitafanya vizuri maana hata darasa la nne nilifanya mitihani ya Taifa, lakini maswali yaliyokuja yalihusisha masomo tuliyosoma darasani, hivyo hata leo itakuwa hivyo hivyo,” amesema Mathayo Msafiri.

Amesema kutokana na jitihada za walimu wao ambazo walizifanya kwa kuwafundisha vipindi vyote na kufanya majaribio mara kwa mara, tayari wameiva vizuri na watafanya vizuri ili kuendelea na kidato cha kwanza mwakani.

Mwanafunzi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Neema amesema amejiandaa kufanya mtihani huo na hana hofu kwa kuwa anaamini kuwa alichojifunza ndicho atakachopimwa.

“Walimu wetu wametuandaa kwa kutufundisha masomo darasani na sisi pia tumejiandaa vizuri, hivyo tunafahamu ya kufanya mtihani wa Taifa ili tusonge hatua inayofuata,” amesema.

Mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, Neema  Com amesema kipimo cha wanafunzi kuelewa walichofundishwa ni kupitia mitihani, hivyo amewataka wahitimu hao kufanya mitihani hiyo kwa umakini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Profesa Said Ally Mohamed, jumla ya watahiniwa 1,172,279 wanatarajiwa kufanya mtihani huo kwa kipindi cha siku mbili.