Unguja. Baada ya kilio, mateso na kuhangaika kwa muda mrefu wakazi wa kisiwa cha Uzi na Ng’ambwa Mkoa wa Kusini Unguja, sasa wameeleza matumaini mapya baada ya kuanza ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilometa 2.2 kuunganisha visiwa hivyo na maeneo mengine.
Kwa kawaida wananchi wa visiwa hivyo kuingia na kutoka hutegemea kupwa na kujaa kwa maji ya bahari, jambo ambalo limekuwa kikwazo sio kwa maendeleo, lakini hata upatikanaji wa huduma kama afya, elimu na zinginezo kutokana na kukosekana kwa wataalamu kuishi katika mazingira hayo.
Shehia hizo mbili zinazounda visiwa hivyo, vina wakazi 4,233 kati ya hao wanawake ni 2,081.
Serikali ya Mapinduzi imeamua kuwaondolea wananchi hao adha kwa kuwajengea daraja kubwa lenye urefu wa kilometa 2.2 likiwa na thamani ya Dola 14.4 milioni za Marekani sawa Sh34.92 bilioni.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 62 na upana wake ni mita tisa urefu wa juu mita nne.
Wakizungumza kuhusu hali hiyo baadhi ya wakazi wa kisiwa hicho wameeleza matumaini yao namna daraja linavyokwenda kuwa mkombozi sio tu wa maisha yao lakini uchumi wao kwa jumla.
Mwanaisha Hassan, mkazi wa kijiji hicho amesema mategemeo yao wanatarajia kupata ahueni ya maisha na kupunguza changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu.
Mwananchi mwingine Khamis Hassan Ali amesema magari yalikuwa yakiharibika kutokana na mazingira kuwa mabovu.
Abdul Said Kahmis kwa upande wake amesema wamelia kilio cha muda mrefu kutokana na changamoto hiyo, lakini kwa sasa wanafarijika kuona kuna jitihada kubwa zinafanyika kuwajengea daraja hilo ambalo litasaidia kuunganisha vijiji hivyo na maeneo mengine.
“Sisi vijana wakati mwingine tulikuwa tunashindwa kucheza mpira, mnapata mashindano kwenda Kibele, Bungi lakini iwapo maji yakishajaa mnashindwa kupita, lakini iwapo daraja hili likikamilika tutaweza kuvuka muda wowote ambao unaweza kupita bila kupata vikwazo vyovyote,” amesema.
“Tunashumkuru Rais Mwinyi (Hussein) alikuja huku akatuambia nabeba jukumu hili nakwenda kulifanyia kazi, kweli tumezana kuona matokeo yake,” amesema.
Zuleikha Haroub Juma mkazi mwingine wa Uzi amesema ujenzi wa daraja hili umeibua faraja kubwa kwao, “tunaona kama inakwenda kuwa neema tupu na kuongeza imani ya kukuza uchumi wetu.”
Abduhalim Issa Ali ambaye ni mfanyabiashara wa samaki kisiwani humo amesema walikuwa hata wakati mwingine samaki zao zinaharibikiwa kutokana na kushindwa kusafirisha mzigo wao.
“Tayari mzigo nimeshaupata nataka niondoke hapa niende mjini, lakini maji yakishajaa nashindwa kusafirisha mzigo, au ukienda sokoni utakuwa umeshachelewa na unapata hasara kwasababu muda unakuwa umeshaisha,” amesema
“Kwa hiyo tunavyotengenezewa hili daraja kwa kweli itabadilisha hata uchumi wetu na maendeleo ya kisiwa hiki yatakuwa makubwa maana hakutakuwa na shida ya kusafirisha mizigo.
Sheha wa Shehia ya Uzi, Othman Haji amesema wananchi wake walikuwa wakipata shida kubwa kwa sababu ya kukosa muunganiko wa kisiwa hicho.
“Tukitoka safari zetu ukikuta maji yameshajaa lazima usubiri maji yatoke, kisha ndio upate fursa kwenda kwenye makazi yetu,” amesema.