INEC yatoa angalizo kauli zinazochochea uvunjivu wa amani

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imeonya wanasiasa wanaotoa kauli kuhamasisha uvunjifu wa sheria kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele alisema hayo Septemba 9, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kauli za baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wagombea wanaohamasisha wananchi kulinda kura.

Jaji Mwambegele alisema kufanya hivyo ni kosa kwani sheria za uchaguzi zipo wazi na wagombea wanafahamu kuwa, zinakataza wasiohusika kubaki kituoni baada ya kupiga kura, badala yake waziache mamlaka halali za kisheria zifanye kazi zake.

“Umeshapiga kura unalindaje, unakuwa kama hauna imani na chombo kinachosimamia. Sheria ipo wazi kuwa hairuhusiwi mtu kukaa ndani ya mita 200 kutoka eneo la kupigia kura. Sasa kama kila mtu atalinda kura si itakuwa fujo,” amesema na kuongeza:

“Sisi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi tunazingatia sheria na miongozo, hakuna mtu atakayeonewa. Matokeo yatakayopatikana ndiyo yatatangazwa. Wanasiasa wanatakiwa waiamini hii ni Tume Huru ya Uchaguzi, ipo huru na itatenda haki.”

Tangu Agosti 28, 2025 zilipozinduliwa kampeni za uchaguzi mkuu wa Rais, wabuge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, baadhi ya wagombea wamekuwa wakitamka hadharani wakiapa kulinda kura zao.

Miongoni mwa kauli hizo ni ya Septemba 7, 2025 iliyotolewa na Kangeta Ismail, ambaye ni Mkurugenzi wa uchaguzi, kampeni na uratibu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho Jimbo la Mbagala, Dar es Salaam alisema: “Safari hii hatuachi kura zetu ziporwe, tumejipanga na tutawapa mbinu ili kuhakikisha tunakusanya hesabu ya kura zetu na matokeo yetu kuyahifadhi tukisubiri kutangazwa.”

Akizindua kampeni Septemba 6, 2025, mgombea ubunge Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema: “Mnafahamu waliyoyafanya mwaka 2020, mwaka huu twendeni tukapige kura na tulinde kura zetu, mwaka huu hatutachezewa, tutashinda na tutatangazwa.”

ACT-Wazalendo imejipambanua wazi katika hilo kupitia kauli yake: “Piga kura, Linda kura,” ikisisitiza si tu kushiriki kupiga kura, bali pia kuhakikisha kura hiyo inalindwa na kuhesabiwa kwa haki, ikihamasisha wananchi kuwa makini na mchakato mzima wa uchaguzi. Inahimiza uwazi, ufuatiliaji wa kura na kulinda matokeo dhidi ya udanganyifu.

Mbali na hao, Septemba 8, 2025, mgombea ubunge wa Ubungo, Dar es Salaam kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kitila Mkumbo akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, alisema kuna mikakati ya kuhakikisha wanajua idadi ya kura zilizopigwa hata kabla matokeo rasmi hayajatangazwa.

“Mifumo ipo, watu wanapewa kazi kuhakikisha matokeo, unakuwa unajua kura zimepigwaje unasubiri tu yatangazwe,” alisema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Onesmo Kyauke anazungumzia hayo kwa kueleza: “Ni kweli katika kampeni za uchaguzi tumeona wagombea wakitangaza mikakati ya kulinda kura zao, binafsi hali hii ina ujumbe mara mbili.”

“Kwanza, inaonesha bado kuna ukosefu wa imani kamili miongoni mwa vyama na wagombea kuhusu mfumo mpya unaosimamiwa na INEC. Kwa maana hiyo, pamoja na mabadiliko ya sheria, bado vyama na wagombea wanajihisi wanapaswa kuwa na mifumo yao ya ndani kuhakikisha kura zao hazipotei,” amesema.

Pili, amesema inaonesha bado kuna changamoto kwa tume yenyewe, zinazohitaji ufumbuzi ili kujenga imani kwa wadau wa uchaguzi.

Amesema wananchi na wadau wakuu wa siasa bado hawajapata uhakika wa asilimia 100 kwamba tume inafanya kazi kwa weledi, uhuru na uwazi wa kutosha.

Dk Kyauke amesema ni wajibu wa INEC kuendelea kujijengea imani ya umma kupitia uwazi wa uamuzi wake, usawa wa kushughulikia malalamiko ya wagombea na uratibu thabiti wa mchakato mzima wa uchaguzi.

“Kwa mtazamo wangu, bado kuna haja ya maboresho zaidi kuhusu utaratibu wa kisheria na Kikatiba kuhakikisha uhuru wa tume unalindwa na hauingiliwi na vyombo vya dola. Pia, uwazi wa kiutendaji mfano, kushirikisha vyama vyote kwa kiwango sawa katika hatua zote za maandalizi na kuhesabu kura, pamoja na kutumia mifumo ya kisasa kama geometric inayozuia udanganyifu na kurahisisha ufuatiliaji wa matokeo,” amesema na kuongeza:

“Elimu kwa umma na mawasiliano itolewe ili wananchi waelezwe kila hatua ili imani kwa tume izidi kujengwa. Kauli za wagombea kuhusu kulinda kura zao zinapaswa kuamsha tume kuona kama kuna pengo la imani ambalo linahitaji kuzibwa kwa vitendo.”

Kwa upande wake, Dk Paul Loisulie amesema uoga wa wanasiasa wa upinzani na wa CCM hauwezi kufanana, akieleza kelele za wapinzani ni kilio cha muda mrefu. “Kura ni kura inawezekana hujuma kutokea, lakini kwa mgombea wa CCM ana wasiwasi gani, wapinzani wao ni kelele za siku nyingi. Jambo linanojitokeza hapa ni kuwa Tume ya Uchaguzi bado haiaminiki kwa wanasiasa na cha msingi ni kuangalia upya mifumo ya uchaguzi ili kumaliza matatizo haya,” amesema.