Kesi ya wanafunzi wa chuo wanaodaiwa kumjeruhi mwenzao, kuanza kusikilizwa leo

Dar es Salaam. Kesi ya kusababisha madhara mwilini inayowakabili mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mary Gervas Matogolo (22) na wenzake wawili, itaanza kusikilizwa leo kwa kutolewa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia, wanadaiwa kupasua simu ya Magnificant Kimario, kuchoma moto nguo alizokuwa amevaa pamoja na pochi ya mkononi, vyote vikiwa na thamani ya Sh1 milioni.

Mary na wanafunzi wenzake  wanakabiliwa na mashtaka nane, likiwemo la kutishia kuua, kutoa taarifa za uwongo mitandaoni na uharibifu wa mali za mwanafunzi mwenzao.

Mbali na Mary wanafunzi wengine katika kesi hiyo ni Ryner Ponci Mkwawili wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam na Asha Suleiman Juma, wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA).

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga na leo Septemba 10, 2025, ambapo imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi baada ya upelelezi kukamilika na washtakiwa kusomewa hoja za awali.

Hata hivyo, washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Kwa pamoja washtakiwa wanadaiwa Machi 14, 2025, eneo la Sinza wilayani Ubungo, Dar es Salaam walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo.

Shtaka la pili  ambalo ni kusabambaza  taarifa za uongo linawakabili  Mary na Asha.

Wanadaiwa kuwa siku hiyo walisambaza taarifa za uongo, katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno kuwa, “Toa  sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi.”

Shtaka la tatu ambalo pia ni kusambaza taarifa za uongo linalomkabili, Ryner peke yake, anadaiwa kuwa siku hiyo alisambaza taarifa hizo kupitia mtandao wa WhatsApp.

Shtaka la nne  ambalo ni kusababisha madhara makubwa, linamkabili Mary peke yake, akidaiwa kuwa siku hiyo alimshambulia Magnificant Kimario kwa kumpiga kichwani na  chuma na hivyo kumsababishia maumivu makali.

Shtaka la tano ambalo ni kusababisha madhara makubwa, ambalo linawakabili washitakiwa wote.

Inadaiwa kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kwa kutumia nguvu walimvuta nywele Magnificati na kusababisha madhara makubwa.

Shtaka la sita na saba, ambayo ni kuharibu mali, pia yanamkabili Mary peke yake.

Inadaiwa kuwa Mary aliharibu laini ya simu na simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000, mali ya Magnificati.

Shtaka la nane  ni kutishia kuua, ambalo linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa siku ya tukio, walimtishia kumuua. Magnificati kwa kutumia kisu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 30, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 13199 ya mwaka 2025.