Dhana ya uhuru wa kufikiri na kutofautiana mawazo ni utamaduni bandia Tanzania. Itikadi tofauti za kisiasa ni mpishano wa mawazo ya namna bora ya kujenga taifa. Tanzania, kutofautiana vyama kuna maana sawa na ufuasi wa Mungu dhidi ya shetani. Ni mapambano ya malaika dhidi ya kizazi cha Ibilisi. Najenga muktadha!
Chama kimoja kinadhani chenyewe ndicho hasa chenye uwakilishi halali wa Watanzania, vingine vyote ni kundi la maadui wa taifa.
Ni Tanzania, mchuano wa demokrasia umekaribisha mapambano ya ukombozi. Chama kinasimama na agenda ya kukomboa taifa. Unajiuliza dhidi ya nani? Watanzania kwa Watanzania. Ni siasa na hoja za umaarufu (populisim).
William Ruto, alifanya siasa za umaarufu na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta. Alijipambanua kama mkombozi halisi wa wananchi wa kawaida.
Akasema serikali yake ingekuwa ya wachuuzi wa mbogamboga (mama mboga) na wasafirishaji kwa kutumia pikipiki (bodaboda).
Miaka mitatu baada ya kushinda kiti, amelazimika kuunda Serikali ya ushirikiano na wapinzani. Ni baada ya kuona nchi ngumu.
Vyama vya siasa vipo kwa ajili ya kushindanisha mawazo. Tanzania imekuwa bahati mbaya. Mfumo wa vyama vingine umekuwa na matokeo ya kujenga makundi ya nchi. Waliopo madarakani wanawaona wanaoyasaka madaraka ni maadui. Wapinzani nao wanawatafsiri walioshika dola sawa na wakoloni. Kisha, wapinzani wao kwa wao, wapo wanaojiona ndiyo wenye uhalali wa kupigania mageuzi, halafu wengine ni wasaliti. Mitazamo hiyo inagawa Watanzania. Watu wanachukiana mithili ya maadui, badala ya kutazamana kama wadau wenye maslahi ya pamoja kwenye nchi.
Ujenzi wa makundi ya ‘No Reforms, No Election’ na ‘Oktoba Tunatiki,’ hayachukuliani kama ni ushindani wa kisiasa kwa ajili ya kujenga taifa moja, bali ni vita mithili ya wafuasi wa Mungu na kizazi cha shetani.
Je, wanasiasa wa Tanzania hawakujifunza kwenye siasa za Seneta John McCain na Rais Barack Obama Marekani? Hawakujionea ushindani wa kisiasa unavyopaswa kwenda kwa kuwatazama Obama na Seneta Mitt Romney? Vyama viwili hasimu, lakini walionesha jinsi ambavyo ushindani wa kisiasa unavyopaswa kuwa baina ya wanasiasa wawili wa nchi moja.
Kipindi cha kampeni za urais Marekani mwaka 2008, mchuano ulikuwa mkali baina ya McCain na Obama. Mmoja ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika, halafu kwa muda mrefu aliishi na kusoma nchini Indonesia, ambayo ni nchi ya Bara la Asia. Akiwa na umri wa miaka sita hadi 10, Obama aliishi Indonesia kwa sababu mama yake, Ann Dunham, aliolewa na mwanaume, raia wa nchi hiyo.
Wazungu wahafidhina walikuwa wakali kila wakiitafakari Marekani chini ya Obama. Waliwasilisha chuki zao moja kwa moja dhidi ya Obama kupitia kwa McCain.
Hata hivyo, hakuna wakati wowote McCain alikubali hoja za kibaguzi dhidi ya Obama. Zaidi, McCain alimtetea Obama mara zote kwamba ni Mmarekani, mtu mzuri, ambaye wametofautiana kisiasa.
Yupo mwanamke alisema Obama ni Mwarabu, McCain akakataa katakata kukubaliana na mtazamo huo. McCain alitaka Obama atambulike kuwa ni Mmarekani halali na mzalendo kwa nchi yake, anayeshindana naye kisiasa. Hakutaka ushindani wao ujenge chuki, kwa sababu Obama ni Mmarekani mwenye haki zote.
McCain alisisitiza: “Obama ni mwanaume baba wa familia, ambaye hakubaliani naye kisiasa.”
Kama McCain kama Romney. Kisha, Obama alishinda urais dhidi ya McCain na Romney. Katika hotuba yake ya ushindi dhidi ya McCain, Obama alisema:
“Muda kidogo jioni hii nilipokea simu kutoka kwa Seneta McCain, ambaye alipambana mno kufanya kampeni. Alipambana zaidi kwa ajili ya nchi anayoipenda.
Amekuwa akijitoa kwa ajili ya Marekani kiasi kwamba hakuna mtu anaweza kuanza kufikiria.
“Wamarekani wamekuwa na hali bora kwa sababu ya huduma ambayo kiongozi huyu jasiri na asiye na ubinafsi amekuwa akiitoa kwa nchi yetu. Nampongeza McCain kwa yote ambayo ameyafanikisha, na ninatazamia kukutana naye kwa ajili ya kuhuisha ahadi za nchi yetu.”
Romney alimpongeza Obama kwa ushindi, halafu akasema kuhusu mkewe, Ann Romney: “Nasikitika sana, Wamarekani wangepata first lady bora kuwahi kutokea kama ningechaguliwa kuwa Rais.”
Obama alimpongeza Romney na familia yake kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitoa kwa ajili ya utumishi wa umma.
“Inawezekana tumepambana sana katika kampeni hizi, ni kwa sababu tunajali sana kesho ya nchi yetu,” alisema Obama akizungumzia mchuano wake na Romney.
Obama, McCain na Romney, wanaweza kuwa mfano bora wa siasa za kistaarabu katika nyakati tulizonazo.
Hawakutaka kufanya siasa za umaarufu. Ni tofauti na Donald Trump, ambaye ameamua kupita katikati ya maisha ya chuki za ubaguzi wa rangi ili kuvuta mtaji wa kisiasa. Amekuwa akifanikiwa, shida ni kwamba siku Marekani ikipata tena kiongozi muunganishaji, kazi itakuwa kubwa kuunganisha taifa. Nilisoma kitabu cha utafiti uliofanywa na taasisi ya Repoa mwaka 2007. Ndani ya kitabu hicho, imeelezwa kwamba kiasi cha Watanzania kutoaminiana ilifikia asilimia 78. Tafsiri yake ni kuwa katika Watanzania 100, ni 22 tu wanaoaminiana. Vilevile katika 10 ni wawili tu.
Mwaka 2007 haukuwa wa uchaguzi. Kipindi hiki Tanzania inakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu, tena ikiwa ni miaka 18 baada ya utafiti wa Repoa, ni rahisi kubashiri bila utafiti kuwa hali ni mbaya. Ukijumlisha na jinsi wanasiasa wanavyoendekeza siasa za umaarufu, yaani kuchafua wenzao na kujipa umalaika, bila shaka, tatizo ni kubwa zaidi.
Kutokana na hali hiyo, wasiwasi ni mkubwa kwamba baada ya Oktoba 29, 2025, inawezekana kukawa na kazi kubwa ya kufanya ili kuiunganisha nchi.
Hakuna siasa za umaarufu zisizo na gharama. Watu waache tamthiliya za kuchafua wenzao na kujipa umalaika. Ushindani uliopo ni baina ya Watanzania, siyo dhidi ya Wakoloni.