WAKATI tamasha la Simba Day likifikia kilele leo, mashabiki wa timu hiyo wamejitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo linafanyika leo likiwa ni msimu wa 17 tangu lilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2009, chini ya uongozi wa Hassan Dalali na Mwina Kaduguda.
Nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, mashabiki wamejitokeza kwa wingi ili kushuhudia kilele cha tamasha hilo lililojizoelea umaarufu mkubwa hapa nchini, tangu lilipoasisiwa kwa mara ya kwanza.
Mashabiki wa timu hiyo wameonekana wakivalia jezi mpya za timu hiyo, huku nyekundu zikitawala zaidi sambamba na bluu na zile nyeupe.
Kwa upande wa hali ya usalama, imeendelea kuimarishwa huku askari wakiendelea kupiga doria maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya uwanja kwa lengo la kulinda mali za raia wote waliojitokeza katika tamasha hilo.
Kwa ndani mambo yanaendelea kwa burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii ikiwamo bendi ya Twanga Pepeta mbali na mechi kadhaa za kirafiki ikiwamo ile ya Simba U2 dhidi ya Misitu FC na maofisa wa Simba dhidi ya Equity Bank.