Vikindu, Mkuranga – Septemba 9, 2025: Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Mariam Abdallah Ibrahim, ameongoza hamasa kubwa ya kisiasa kwa kuwaomba wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025 na kuwapigia kura wagombea wote wa CCM ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa chama hicho.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mariam alisisitiza kuwa mshikamano wa wananchi na viongozi wa CCM ndio nguzo ya kuendeleza maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alimuombea kura Rais Samia, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga Abdallah Ulega, pamoja na Mgombea Udiwani wa Kata hiyo Mohamed Maundu.
“Tarehe 29 Oktoba tusifanye makosa, tupige kura kwa Rais wetu Dkt. Samia, tumchague Mbunge wetu Ulega na Diwani wetu Maundu, ili tuendelee na kazi nzuri ya maendeleo ambayo tayari tunaiona hapa Vikindu na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani,” alisema Bi. Mariam huku akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa Vikindu, Mohamed Maundu, alitumia fursa hiyo kueleza utekelezaji wa miradi kadhaa iliyofanikishwa katika kipindi chake cha uongozi, ikiwemo upatikanaji wa umeme vijijini, ujenzi wa shule za msingi mpya, vituo vya afya na zahanati pamoja na barabara za lami.
Maundu aliwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia, sambamba na kumchagua Rais Samia na Mbunge Ulega, akisisitiza mshikamano na mshirikiano kati ya viongozi na wananchi kuwa ndiyo msingi wa maendeleo endelevu.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionesha hamasa kubwa, wakiapa kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kuipa CCM ushindi wa kishindo.